SERIKALI imesema haitasita kuwachukulia hatua kali
za kisheria wafanyabiashara wote kutoka nje wanaofanya biashara au kufungua
viwanda vidogo vidogo bila kufuata taratibu, kanuni na sheria za nchi. Moblog
inaripoti.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika
kuadhimisha Siku ya Viwanda Afrika jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Bi. Maria Bilia amesema kuna baadhi ya
wafanyabiashara toka nje ambao hawataki kufuata taratibu za uwekezaji na sheria
za nchi.
“Matokeo ya kutokufuata sheria za nchi katika
uwekezaji au ufanyaji wa biashara ni uanzishwaji wa viwanda vinavyozalisha
bidhaa ambazo hazikidhi viwango na ni hatari kwa Afya za walaji,”
“Sheria za nchi zipo wazi kwamba lazima Kituo cha
Uwekezaji (TIC) na Brela msajili wa biashara wahusishwe kwenye mchakato mzima
wa uwekezaji au biashara yeyote ndani ya nchi,” Bilia amesema
Amesema vile vile Wizara ya Viwanda kwa
kushirikiana na Wizara zingine na taasisi za Serikali wanaendelea kurahisisha
urasimishaji wa biashara kwa wanyonge kupitia mradi wa Mkurabita Mkakati wa
Kurasimisha Biashara kwa Wanyonge ili kuwawezesha wazawa kufanya biashara zenye
tija kwao na taifa kwa ujumla.
Bi. Bilia aliendelea kusema kuwa siku ya viwanda
Afrika ilianzishwa mwaka 1989 na Tanzania ilijiunga rasmi mwaka 1990 katika
kuhamasisha ukuaji wa viwanda katika kukuza uchumi wa nchi za Afrika.
Amesema sekta ya viwanda ikishirikishwa na sekta
zingine inaweza kufanya mabadiliko haraka katika maisha ya mtu mmoja mmoja
hususani ajira na hutoa bidhaa bora kwa matumizi ya binadamu.
Alisisitiza kuwa mwaka huu Serikali imepanga kuwa
na maonyesho ya wiki nzima yatakayofikia kilele tarehe 20 mwezi huu ambapo
wafanyabiashara mbalimbali watapata fursa ya kuonyesha bidhaa zao katika ukumbi
wa PTA saba saba.
Amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni “ Ni Ajira na
ujasiriamali, Fursa ya Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda Afrika katika juhudi za
kupunguza makali ya umaskini na tatizo la ajira kwa vijana.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Shirikisho la
Viwanda Nchini (CTI) Dkt. Samwel Nyantahe amesema shirikisho la viwanda
linaunga mkono juhudi za serikali katika kuongeza thamani ya bidhaa
zinazozalishwa hapa nchini ili kuongeza mapato ya nchi.
Bw. Gerald Runyoro kutoka Shirika la Umoja wa
Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) amesema umoja wa mataifa kwa
kushirikiana na serikali na wadau wengine wataendelea kusisitiza watu kuwekeza
na kufungua viwanda ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi Afrika.
Amesema wafanyabiashara lazima wawe na ujasiri wa
kufungua biashara au kiwanda katika juhudi za kuongeza thamani bidhaa zitokazo
Afrika na kutafuta fursa za uwekezaji nje ya Afrika.

No comments:
Post a Comment