Taifa Stars sasa
inacheza na Zimbabwe mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA)- FIFA Date itakayofanyika keshokutwa Jumanne (Novemba 19 mwaka
huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilikuwa icheze na Kenya (Harambee
Stars), lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) lilituma taarifa jana
jioni (Novemba 16 mwaka huu) likieleza kuwa timu yake haitacheza tena mechi
hiyo.
Kikosi cha Zimbabwe
chenye msafara wa watu 30 kinatarajia kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) kesho (saa 3 asubuhi) tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa
kuanzia saa 11 kamili jioni.
Waamuzi wa mechi
hiyo wanatoka Uganda wakati Kamishna atakuwa Leslie Liunda wa Dar es Salaam.
Mwamuzi wa mezani ni Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam.
Stars chini ya Kocha
Kim Poulsen ipo kambini tangu Novemba 12 mwaka huu kujiwinda kwa mechi hiyo.
Kim amejumuisha kwenye kikosi chake wachezaji watano wanaocheza mpira wa miguu
nje ya Tanzania.
…5,000/- NDIYO
KIINGILIO CHA KUISHANGILIA STARS
Kiingilio katika
mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya wenyeji Tanzania (Taifa Stars) na
Zimbabwe ni sh. 5,000 wakati tiketi zitaanza kuuzwa Jumatatu (Novemba 18 mwaka
huu) kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Mbali ya kiingilio
hicho cha sh. 5,000 ambacho ni kwa viti vya bluu na kijani, viingilio vingine
ni sh. 30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B, sh. 15,000 kwa VIP C wakati viti
vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000.
Tiketi zitauzwa
katika magari maalumu katika vituo vya; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa,
mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, Sokoni Kariakoo, Dar Live
Mbagala, OilCom Ubungo, BMM Salon iliyopo Sinza Madukani, Uwanja wa Uhuru,
mgahawa wa Brake Point uliopo Kijitonyama, na kituo cha mafuta Buguruni.
Boniface
Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu
Mkuu
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:
Post a Comment