KIKWETE ATOA ANGALIZO
RAIS Jakaya Kikwete ambaye ni
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema tatizo la rushwa ndani ya chama
hicho lisipodhibitiwa litakiondoa chama hicho madarakani.
Amesema chama hicho kikishinda
katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na tatizo la rushwa likaendelea, litakifanya
chama hicho kutoshinda tena katika uchaguzi wa mwaka 2020.
“Tukiendelea hivyo, tukishinda
uchaguzi ujao wa mwaka 2015 ni bahati, lakini tukifanikiwa kupenya uchaguzi wa
mwaka 2020 hatutoki,” alisema.
Alisema hayo juzi mjini hapa wakati
akifunga mafunzo maalumu ya watendaji wa wilaya na mikoa wa CCM na kumpa rungu
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kuwashughulikia viongozi wala
rushwa ndani ya chama hicho.
“Tusipoangalia hili la rushwa
tutaiondoa madarakani CCM na mambo yote mazuri tuliyofanya hayataonekana, hapo
lazima wananchi watawauliza je, ugonjwa huu mmeshindwa kuachana nao, basi
tumeamua kuwapumzisha,” alisema.
Mwenyekiti wa chama hicho kilicho
madarakani tangu Tanzania ipate uhuru, alisema rushwa itaizika CCM kwani hiyo
ni hila ambayo itakifanya chama hicho kishindwe kuongoza kwa muda mrefu.
“Acheni kuvutavuta, mtu anarushiwa
Sh 200,000 ya air time (muda wa maongezi wa simu ya mkononi) hiyo ni nini
acheni hicho kitu,” alisema na kuongeza kuwa tatizo la rushwa limewachosha
wananchi na kutishia chama kuendelea kuongoza.
Alisema wanaotoa fedha ndio
wanapokewa kwa shangwe na viongozi hao ndio wamekuwa wakiwatafutia watu
ushindi, kitu ambacho wananchi wamekichoka na kuwa na chuki na chama hicho.
“Nakupa Mangula (Phillip) rungu la
kuhangaika nao,” alisema Rais Kiwete huku akishangiliwa na wajumbe hao wa
mkutano.
Alisema dawa ya viongozi kama hao ni
kuachana nao kwani kuna makada wengi ambao hawana makandokando lakini wale
wenye maradhi hayo chama hakiwezi kuendelea nao.
“Njaa taabu sana, ukiendekeza sana
njaa ndiyo inakuwa hivyo, utu unakutoka, tusifanye hivyo chuki ya watu kwa
rushwa ni kubwa, kiongozi kuwa wakala wa kusambaza fedha ni aibu kama unatosha
utapita tu,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yatasaidia
kuweka sawa ng’we ya pili ya awamu ya nne ya serikali ya CCM na kutekeleza kwa
vitendo kaulimbiu ya ushindi ni hakika katika uchaguzi wa serikali za mitaa
2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Alisema lengo kuu la CCM kama ilivyo
kwa vyama vingine vya siasa ni kushika dola na CCM ipo kwa ajili ya kutawala
lakini mtu akitoka kwenye lengo hilo akatafute shughuli nyingine ya kufanya sio
hiyo kwani dhumuni kuu ni kushika dola.
Alisema pamoja na majukumu mengine
ni lazima kuhakikisha wagombea wa CCM wanashinda na kuendelea kukamata dola na
kama viongozi na watendaji wakuu ni kutambua na kuhakikisha chama kinakuwa na
nguvu ya kutosha ili kufikia kwenye lengo kuu.
Aliyataja mambo matatu ambayo
yakifanyika, CCM itakuwa na nguvu. Mambo hayo ni kuimarisha chama, tabia na
mwenendo mzuri wa viongozi na wanachama na utendaji mzuri wa viongozi wa CCM.
Alisema wakifanya hayo chama
kitakuwa na nguvu na kila mgombea watakayemweka atasubiri kuapishwa kwani
kutakuwa hakuna wa kumpinga na hilo litawezekana iwapo chama kitakuwa na uhai
kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya Mkoa hadi taifa.
Pia aliwataka kutunza wanachama
waliopo ambao wataendelea kukaribisha wenzao ili chama kiwe na nguvu kwani
wingi wa wanachama ni mtaji wa kutafuta ushindi.
“Ukiwa na wanachama milioni sita
waaminifu hii itafanya mgombea wako kuwa na kura milioni sita za kuanzia, kazi
yenu ni kuhakikisha tunashinda kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura,”
alisema.
Aliwataka kuweka mikakati ya
kutembelea wanachama katika maeneo yao ya uongozi ili watu wajue wenyewe wapo
na kama viongozi wakiogopa kukutana na wanachama, chama hakitashinda.
“Badilikeni kama matawi yako huyajui
mnataka uongozi tu na ingekuwa mnaitwa kwa usaili siku hiyo ingekuwa ni aibu
maana mnaongoza watu msiowajua,” alisema.
Alisema vyama vya upinzani vimekuwa
vikifanya kazi hiyo kwani hata wakiomba barua kwa makamanda wa polisi ya orodha
ya barua ya vyama vya siasa vilivyoomba kufanya mikutano, CCM haimo.
Alisema wapinzani wanazunguka ndiyo
maana hata bendera ziko nyingi na wamekuwa wakizungumza na watu na wamekuwa
wanafanya kazi ya kutembea ambayo CCM hawaifanyi.
“Mnasubiri wakati wa kampeni wakati
watu wakiwa wamejazwa maneno mengi hata muda wa kujitetea unakuwa hakuna na
matokeo yake chama kinashindwa kwenye uchaguzi,” alisema.
Pia alishutumu baadhi ya viongozi
kutumia vibaya rasilimali za chama, ikiwemo kuuza viwanja na hata kupangisha
kwa mikataba yenye utata.
Akitoa mfano alisema kuna mtu
kapangishwa jengo la CCM kwa miaka 264 kitu ambacho ni aibu kubwa. Awali,
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema jumla ya mada 19 zilitolewa
katika maeneo yote muhimu ndani ya chama na nje ya chama.
Alisema mafunzo hayo yalihusu
maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2014 na mwakani yatafanyika
mafunzo kama hayo kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2015.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa(
NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema mafunzo hayo maalumu yalihusisha
wilaya 161 za Tanzania bara na Zanzibar ambapo wajumbe 426 walihudhuria kati ya
wajumbe 443 waliotarajiwa ikiwa ni sawa na asilimia 96.2.

No comments:
Post a Comment