KENYA YAITEGA UN
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Kenya imewasilisha rasmi barua kwa Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa kuahirisha kesi zinazoendelea katika mahakama ya ICC dhidi ya
rais Uhuru Kenyatta na naibu rais William Ruto. Pia, nchi 49 za Umoja wa Afrika
zimetia saini barua iliyowasilishwa Jumanne kwa baraza hilo ikiunga mkono
kuahirishwa kwa kesi hizo dhidi ya viongozi wa Kenya.
Akizungumza na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika Jumatano, balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa bw. Macharia Kamau alisema Kenya na Umoja wa Afrika wanasubiri kwa hamu maamuzi ya Baraza hilo.
Balozi Kamau alisema Kenya inakabiliwa na tishio kuu la ugaidi na ukosefu wa usalama hata kutoka pembe ya Afrika. Alisema ombi la Kenya la mwaka wa 2011 katika Baraza hilo halikupata majibu yaliyotegemewa na kwamba viongozi wake bw. Kenyatta na naibu rais Ruto wanahitaji kuwa nchini kusimamia shughuli za usalama na majukumu yao kama wanavyotakiwa na katiba ya nchi hiyo.
Viongozi hao wa Kenya wanakabiliwa na mashtaka mbele ya mahakama ya kimataifa ya ICC kwa tuhuma kwamba walichochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007 na mapema mwaka wa 2008.

No comments:
Post a Comment