Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ameridhia utozwaji wa faini ya dola za
kimarekani laki tatu na nusu sawa na shilingi milioni mia saba na sabini
iliyotozwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu (DSFA) kwa Meli ya Buah
Naga 1 kutoka nchini Malaysia kwa kosa la kukutwa mapezi ya
samaki aina ya papa kilo 90 huku miili ya samaki hao kutupwa baharini kinyume
na kanuni ya 66 ya kanuni za bahari kuu za mwaka 2009 na kifungu namba 18(2)
cha Sheria yaUsimamizi wa Bahari Kuu(DSFA) ya Mwaka 1998 kama
ilivyorekebishwa Mwaka 2007.
Akizungumza baada ya kukagua meli hiyo mjini Mtwara, Waziri Mpina
alisema kuwa wamiliki wa meli hiyo wanatakiwa kulipa faini hiyo
ndani ya siku saba ambapo kama hawatalipwa watapelekwa mahakamani mara moja na
kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Aidha Mpina amesema Serikali imetaifisha tani nne na nusu za samaki ambazo
zitauzwa mara moja kwa njia ya mnada na kwa kuzingatia taratibu mbalimbali za
Serikali.
Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa meli hiyo, kwa Waziri, Kiongozi wa
Kikosi Kazi maalum cha kudhibiti uvuvi haramu, Kamishna Frederick Milanzi
wa Tume ya Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini amesema kwamba Kapteni wa meli
hiyo Han Ming Chuan raia wa Malaysia alikutwa na bastola aina
ya Bereta na risasi kumi ambayo alikuwa anaimiliki kinyume cha sheria.
Amesema kuvua na kutupa mizoga ya samaki baharini siyo tu kwamba
wanahujumu raslimali za uvuvi baharini bali pia wanachangia katika
uchafuzi wa mazingira ya baharini.
Pia Waziri Mpina amesisitiza kuwa Serikali haipo tayari kufanya
kazi na wawekezaji wababaishaji kwenye sekta ya uvuvi na kwamba
kuanzia sasa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote
atakayejaribu kuhujumu raslimali za uvuvi na kujihusisha na uvuvi haramu.
Aidha Waziri Mpina ametoa onyo kali kwa wawekezaji wa uvuvi
kwenye bahari ya Tanzania kuacha kutumia mwanya wa kupewa kibali cha kuvua na
kujihusisha na makosa mbalimbali.
Ameyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ni pamoja na
usafirishaji haramu wa silaha, binadamu, madawa ya kulevya na nyara za serikali
ikiwemo meno ya tembo. Pia usafirishaji wa mazao ya misitu na samaki.
Kwa upande wake, Bw. Wankyo Simon ambaye ni Wakili wa Serikali kutoka
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Divisheni ya Mashtaka Makao Makuu Dar es
Salaam na Mkuu wa Dawati linalohusiana na Makosa ya Mazingira, amesema makosa
ya namna hii ni makubwa na endapo kiwango hicho cha pesa hakitalipwa kama
ilivyoamriwa, taratibu za kiupelelezi zitakamilishwa na kapteni wa Meli hiyo
atafikishwa mahakamani kwa makosa yaliyoainishwa ambapo anaweza kupewa adhabu
ya kifungo na meli hiyo kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.
Pia amependekeza kuwepo kwa mwongozo wa uendeshaji mashauri (Standard
Operating Procedures) kwa makosa yanayofanyika baharini ili uweze kutumiwa na
wadau mbali mbali kuanzia ukamataji wa chombo husika, upelelezi wake, namna
bora ya kutunza chombo hicho na uendeshaji wa mashauri yanayotokana na
operesheni zote zinazofanyika baharini.
Alisema mwongozo utasaidia kuimarisha kesi zote zinazoenda mahakamani
kuanzia inapofunguliwa mpaka kufikishwa mahakamani na wadau wote watajua kwa
urahisi namna ya kusimamia utekelezaji wa majukumu yao.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa (DSFA) Hosea Mbilinyi amesema Mamlaka yake
imegundua kuwepo kwa baadhi ya wawekezaji wasiofuata taratibu na
Sheria za kufanya shughuli za uvuvi katika bahari ya Tanzana ambapo
amesema tayari Mamlaka imeshawapiga faini ya dola za kimarekani laki moja kwa
meli tatu zilizofanya makosa katika sikuza hivi karibuni.
Katika siku za hivi karibuni Waziri wa Mifugo na Uvuvi ameunda timu
iliyoshirikisha wataalam kutoka katika vyombo mbali vya Serikali
kuendesha operesheni maalum ya kutokomeza uvuvi haramu nchini ambayo
licha ya kupata mafanikio makubwa imetoa hamasa kwa wavuvi kuanza
kusalimisha zana haramu za uvuvi na kuziteketeza.
No comments:
Post a Comment