
WILAYA YA MUHEZA, TANGA, TANZANIA –
Katika sherehe zilizofanyika katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Shirika la
Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) yaligawa tableti zilizowekewa
mfumo wa elimu kwa watoto.
Tableti
hizo ziligawiwa kama sehemu ya mradi wa majaribio wa miezi 15 chini ya Global
Learning XPRIZE, ambao ni mradi wa miaka mitano uliotokana na mashindano
duniani yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 15.
Mradi huu
wa dunia unatoa changamoto kwa timu za wabunifu kubuni na kuandaa zana- wazi za
kiteknolojia ili kuwawezesha watoto walio na fursa ndogo ya kupata elimu katika
umri wa miaka tisa hadi kumi na mmoja, kujifunza wenyewe stadi za msingi za
Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Kama sehemu
ya majaribio, zaidi ya watoto 2,400 kutoka katika vijiji 167 katika wilaya za
Handeni, Korogwe, Lushoto, Mkinga, Muheza, na Pangani watapewa tableti mpya ya
aina ya Google Pixel C, zilizotolewa kwa hisani ya Google. Tableti hizo
zimewekewa mifumo ya elimu kutoka kwa washindi watano wa mwisho wa Global
Learning XPRIZE.
Washindi
hawa walichaguliwa kutoka katika timu 198 na paneli ya majaji 11 wa kujitegemea
na walio wataalamu na kutangazwa mwezi September, 2017 wakati wa wiki ya Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa.
“Teknolojia
hii inayowawezesha watoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu pasipo msaada
wa mwalimu, ni ubunifu wa kiwango cha juu kabisa,” alisema Mayasa Hashim ambaye
ni Afisa Elimu Mkoa wa Tanga. “Msaada huu utaleta matokeo mazuri katika
kuwakomboa watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ili kwamba na wao wajifunze
stadi hizi.”
Tableti
hizo ziligawiwa na WFP kwa sababu shirika hili linasimamia uendeshaji wa
kitengo cha lojistiki na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) cha
majaribio katika mazingira halisi. Jukumu lake ni pamoja na kuingiza zana hiyo
ya kiteknolojia katika tableti, kuanzisha vituo vya kuwekea umeme unaotokana na
jua kwenye tableti hizo vijijini na kusimamia matengenezo, marekebisho na kutoa
tableti mpya katika kipindi chote cha majaribio ya ugani.
“Ubunifu
katika teknolojia unaweza kuwa jibu kwa baadhi ya changamoto kuu duniani,”
alisema Mwakilishi wa Nchi wa Shirika la WFP Tanzania Michael Dunford.
“Majaribio haya yanamaanisha kwamba tunaweza kutumia teknolojia mpya ili
iwahudumie watoto wasio katika mfumo rasmi wa elimu pamoja na watu wengine
walio hatarini—na hivyo kuhamasisha uletaji wa maendeleo zaidi katika mchakato
huo.
Ubunifu wa
aina hii unafungulia milango kwa Serikali, mashirika na biashara kuendeleza
katika modeli ambazo zimekwishajaribiwa tayari na kuvunja mwiko wa ukomo katika
yale tuliyodhani ndiyo pekee yanawezekana, na si tu katika sekta ya elimu bali
pia katika maeneo mengine ya maendeleo ya watu.”
Upande wa
elimu katika majaribio ya ugani unasimamiwa na UNESCO kwa kushirikiana na
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Vilevile, UNESCO ina wajibu wa kusimamia
maendeleo ya watoto katika Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ili kuweza kupima ni
zana ya mshindi yupi wa mwisho ilileta matokeo bora zaidi.
“Mradi huu
unaendana na majukumu ya UNESCO katika kuhamasisha elimu jumuishi, itolewayo
kwa usawa wenye haki na iliyo bora, na wakati huohuo kuchangia kwa kiasi
kikubwa katiak juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali wa elimu nchini Tanzania
katika kuhakikisha watoto wote, wakiwemo wale wa jamii za pembezoni na zilizo
nyonge, kupata fursa sawa katika elimu,” alisema Msimamizi wa UNESCO Faith
Shayo.
“Mradi huu
unawapa watoto ambao hawakuwahi kujiunga na shule ya msingi pasipo sababu fursa
nyingine, huku lengo kuu la kuwapa fursa ya kuingia au kuingia upya katika
mfumo rasmi wa elimu ni baada ya kukamilika kwake. Hii inaonyesha juhudi kubwa
za pamoja kati ya Umoja wa Mataifa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha
viwango vya kujua kusoma na kuandika miongoni mwa vijana wa kizazi kipya nchini
kwa kutumia teknolojia zinazotokana na ubunifu, zinazoweza kusambazwa kwa wingi
na zenye gharama nafuu. Mradi huu unaweza kupanuliwa na hatimaye kuenewa katika
mikoa yote ya Tanzania, ili kuendeleza ujifunzaji katika elimu ya awali.”
Mwisho wa
awamu ya majaribio ya ugani, timu ya washindi wa mwisho ambao masuluhisho
waliyotoa yana tija zaidi watapata zawadi kubwa ya Dola za Marekani milioni 10.
Mshindi atatangazwa mwezi Aprili, 2019. Kufuatia mashindano, kila washindi wa
mwisho watano wataweka huru zana zao na maudhui yake ili zipatikane bure na kwa
yeyote mwingine kuona namna ya kuzipanua. Inatarajiwa kwamba njia hii ya
kujifunza mwenyewe itawaongoza kujifunza na hatimaye kuwawezesha watoto kote
nchini Tanzania kuwa na umiliki zaidi wa elimu yao.
Sherehe
itafanyika mapema mwaka 2018 ili kuadhimisha kuanza kwa majaribio haya ya
ugani. Sherehe hizo zitaandaliwa kwa kushrikiana na Serikali ya Tanzania,
UNESCO, WFP na Global Learning XPRIZE.
No comments:
Post a Comment