Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ibaga, Wilaya ya Mkalama mkoani Singida,
wakati wa ziara yake hivi karibuni kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
Serikali
imeliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha wateja wote
walioomba na kulipia huduma hiyo mwaka 2017 wanaunganishiwa kabla ya Desemba 30
mwaka huu.
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alitoa agizo hilo kwa nyakati tofauti hivi
karibuni, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme
mkoani Singida na Dodoma.“Agizo hili ni kwa nchi nzima. Hakikisheni wateja
waliowasilisha maombi yao na kulipia ndani ya mwaka huu wa 2017 wawe
wameunganishiwa umeme siyo zaidi ya Desemba 30 mwaka huu.”.
Aidha,
Dkt Kalemani aliwaagiza watendaji wa shirika hilo kutoa elimu kwa umma, hasa
wananchi walioko vijijini kuhusu umuhimu wa kutumia umeme ili kuwahamasisha
kuunganisha nishati hiyo katika makazi yao.
Akifafanua,
Waziri alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa baadhi ya wananchi hawajaunganisha
umeme katika makazi yao japokuwa tayari Serikali imekwishawafikishia nishati
hiyo katika maeneo yao.“Inawezekana baadhi ya wananchi hawajatambua umuhimu wa
kutumia umeme, hivyo ni vema wapatiwe elimu husika. Tuwatembelee mahali waliko,
hususan vijijini na tuwapatie elimu hiyo,” alisisitiza.
Akizungumzia
faida za umeme, Waziri Kalemani alisema umeme ni kichocheo kikubwa cha
maendeleo kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinahitaji nishati hiyo.Aliongeza
kuwa, ili dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda ifanikiwe,
ni lazima kuwepo na umeme wa kutosha na wa uhakika. “Ndiyo maana tumedhamiria
kufikisha umeme hadi vijjijini kwa kasi kubwa, hivyo wananchi tafadhali tumieni
umeme ili kukuza pato lenu na uchumi wa nchi kwa ujumla.”.
Waziri
aliwapongeza viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya,
Wabunge na Watendaji wa Halmashauri na Vijiji, kwa jitihada zao za kufuatilia
utekelezaji wa ahadi za serikali kwa wananchi ikiwemo upelekaji wa umeme
vijijini.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutunza
miundombinu ya umeme katika maeneo yao ili isihujumiwe na hivyo kuwakosesha
huduma hiyo muhimu na pia kuleta hasara kwa serikali.
Ziara
hiyo ya Waziri Kalemani ni muendelezo wa ziara mbalimbali ambazo amekuwa
akifanya nchi nzima kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na
wananchi wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na kupokea kero na changamoto
mbalimbali za wananchi kuhusu sekta ya nishati ili zifanyiwe kazi.
Katika ziara hii, Waziri ametembelea Wilaya za Mkalama na Singida
Vijijini mkoani Singida pamoja na Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment