Watu wawili wakazi
wa jimbo la Singida Kaskazini mkoani Singida, wamefariki dunia baada ya kuugua
ugonjwa hatari wa Kipindupindu unaotokana na uchafu.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi jana ofisini kwake, Mkuu wa wilaya ya Singida,
Elias Tarimo, alisema Novemba, 26 mwaka huu, ugonjwa huo wa Kipundupindu
ulibainika katika vijiji vya Merya na Msange jimbo la Singida kaskazini.
Hata
hivyo, alisema kuwa ilichukua muda mrefu mno mamlaka zinazohusika kutoa taarifa
ya ugonjwa huo, kitendo kilichochangia idadi ya wagonjwa kuongezeka na kufikia
30.
“Urasimu
huu umesababisha hatua stahiki za kudhibiti ugonjwa huu, kuchelewa kuchukuliwa
na hivyo kuchangia wananchi wawili kupoteza maisha. Kwa sasa tumebakiwa na
wagonjwa sita kambi ya Merya na Msange wapo watatu,” alisema Tarimo.
Mkuu
huyo wa wilaya, alisema baada ya kupata taarifa hizo kwa kuchelewa, hawakulala
walipiga kampeni ya nguvu kuhimiza usafi wa mazingira, matumizi bora ya vyoo na
kuchemsha maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
“Aidha,
wataalam walipima maji ya visima 14 yanayotumiwa na wananchi wa vijiji hivyo,
na 12 kubainika vina vidudu vinavyochangia ugonjwa wa kipindu pindu. Baada ya
kugundua hivyo, tumepiga marufuku maji ya visima hivyo kutumika,” alisema.
Akifafanua,
alisema wamewaelekeza wananchi kutumia maji ya bomba na wamechukua mashine
kubwa ya kupampu maji kutoka kijiji cha Sagara.
“Mashine
hii tumeisimika na itasambaza maji ya bomba katika vijiji hivyo vya Msange na
Merya. Hatujaishia hapo, tunaendelea kuwahimiza wananchi kutumia vidoge vya
waterguird kwa ajili ya kutibu maji yawe safi na salama. Vile vile tanawahimiza
kutumia vyoo na kuacha tabia ya kujisaidia ovyo kwenye vichaka,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Tarimo alisema kuwa baada ya kufanya kampeni ya kuhimza usafi,
mwananchi yoyote atakayeugua Kipindupindu, atatibiwa na akipona, mara moja
atafikishwa mahakamani, kujibu tuhuma ya kutaka kujiuawa kwa makusudi.
Wakati
huo huo, katika kuchukua hatua kudhibiti Kipindupindu, Manispaa ya Singida
imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo ya kupiga marufuku wafanyabiashara wa
matunda, kumenya matunda. Imeagizwa kuwa matunda yote yaliwe nyumbani baada ya
kuoshwa vizuri kwa maji.
Pia
kila kaya imeagizwa kutumia vyoo bora na kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula
chakula na baada ya kutoka chooni.
Mkurugenzi
wa manispaa hiyo, Bravo Kizito Lyapembile, amesema mtu ye yote akikamatwa kwa
kuchafua mazingira, atatozwa faini kati ya shilingi 30,000 na 300,000.

No comments:
Post a Comment