Serikali
ipo katika mkakati wa kuwabana wanafunzi wanaopewa mikopo katika fani za
kipaumbele, kutumikia katika utumishi wa umma nchini kwa muda fulani ili
kuhakikisha dhamira ya serikali ya inatimia.
Fani hizo ni sayansi za tiba na
afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo,
mafuta, gesi asilia, sayansi asilia, mabadiliko ya tabia nchi, sayansi za
ardhi, usanifu majengo na miundombinu.
Serikali inachukua uamuzi huo, baada
ya kubaini kuwapo wanafunzi wanaosomea fani hizo ili kupata mikopo, lakini
baada ya kumaliza hukimbilia kufanya kazi nyingine au nje ya nchi na hivyo
kuendelea kuwepo upungufu wa wataalamu waliowakusudia kubaki.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na mafunzo ya ufundi, Stella Manyanya (pichani) aliyasema hayo hivi karibuni,
alipozungumzia utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Alieleza kuwa
serikali inafikiria kuwe na utaratibu kwa wanaonufaika na mikopo ya kipaumbele
kuingia makubaliano na serikali.
Alisema suala hilo halitakuwa jipya
kwani hapo nyuma walikuwa wakibanwa kuwa lazima kufanya kazi angalau kwa miaka
mitano serikalini na baadaye ni ruhusa kwenda popote, lakini kwa sasa hawawezi
kuwabana wote, lakini lazima kufanya hivyo kwa hao wa kipaumbele.
Aidha Manyanya alizungumzia ulipaji
mikopo hiyo na kudai wanaboresha sheria ya kukusanya madeni kwa kushirikiana na
waajiri.
“Serikali itakusanya madeni hata kwa
wakopaji ambao wamejiajiri kwa sababu wengi wakimaliza masomo hawafikirii
kulipa,” alisema.”Sasa lazima walipe, wakopaji watambue fedha hizo ni mikopo na
lazima kulipa.”
Alisema kwa wakopaji watakaoajiriwa,
wizara inataka mkopo huo kuwa wa kwanza kukatwa kabla ya mingine ili kuepuka
kuingiliana na sheria za kazi, zinazotaka mkopaji kuachiwa fedha fulani katika
mshahara wake.

No comments:
Post a Comment