KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa
imeomba Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imuombe Rais atoe
kibali cha ajira kwa walimu kukabili uhaba unaoikabili nchi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson
Rweikiza alitoa ushauri huo jana mjini Dodoma kwenye kikao kati ya wajumbe wa
kamati hiyo na viongozi na watendaji wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa wakiongozwa na Naibu Waziri, Selemani Jafo.
Kikao hicho kilikuwa ni cha kamati
kupokea na kujadili taarifa .ya tathmini ya utekelezaji wa mpango wa ofisi hiyo
wa utoaji elimu bila malipo katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu
ambako suala la uhaba wa walimu liliibuliwa na wajumbe.
“Walimu waajiriwe...ni
vyema mumuone rais, angalau afungulie kibali cha walimu pekee...wanafunzi
wanaongezeka mara mbili, lakini walimu hakuna,” alisema Rweikiza.
Awali, akijibu hoja za wajumbe juu
ya changamoto ya uhaba wa walimu, hususan wa Sayansi na Hisabati, Jafo alikiri
hali hiyo kuikumba serikali na kusema ndiyo maana walilenga kutoa ajira 35,000
kabla ya rais kusimamisha vibali vya ajira kwa watumishi wote.
Hata hivyo, alisema uamuzi wa Rais
ni wa nia njema kuwezesha uhakiki wa watumishi hewa.Alisema katika kauli ya
hivi karibuni ya Rais John Magufuli, alisema wakati wowote kibali kitatolewa.Jafo
alisisitiza kuwa kibali kitakapotolewa, kipaumbele itakuwa ni ajira kwa walimu
wa Sayansi ya Hisabati.
Akielezea namna ya kuziba mapengo ya
walimu wa masomo hayo, Jafo alisema serikali itafikiria pia watu wengine
wanaoweza kufaa katika kufundisha masomo hayo wakiwemo walimu wastaafu na
wahitimu wa fani nyingine.
No comments:
Post a Comment