
JESHI la Kujenga Taifa
(JKT), limetoa siku saba kwa wabunge wa majimbo 18 yaliyopo ndani ya mikoa saba
nchini kuhakikisha wanachukua madawati yao yaliyotengenezwa na jeshi hilo kabla
ya Agosti 30, mwaka huu.
Madawati hayo 9,666 ni kati ya
30,000 ya awamu ya kwanza yaliyotengenezwa na jeshi hilo baada ya Ofisi ya
Bunge kulipa zabuni ya kutengeneza madawati 60,000 kwa Sh bilioni tatu.
Akizungumza Dar es Salaam jana,
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JWTZ), Dk Hussein Mwinyi, alisema
jeshi hilo limelikabidhi Bunge madawati 30,000, lakini madawati 9,666 kati ya
hayo hayajachuliwa.
Hata hivyo, alisema kulingana na
mgawo ambao jeshi hilo lilikabidhiwa na Kamati ya Bunge, madawati hayo
yaligawanywa katika majimbo ya mikoa tisa, lakini hadi sasa majimbo 18 katika
mikoa saba hayajachukua madawati hayo.
Aliitaja mikoa iliyopo kwenye mgawo
huo na idadi ya madawati kwenye mabano kuwa ni Tanga ( 6,444), Njombe (3,222),
Iringa (3,790), Mbeya (3,759), Mbeya Songwe (3,222), Rukwa (1,611), Ruvuma
(4,833), Unguja (3,200) na Pemba (1,800).
“Mpaka sasa madawati
yaliyokwishachukuliwa ni 22,721, madawati 9,666 kati ya 30,000
yaliyokwishakamilika sawa na asilimia 30 hayajachukuliwa na majimbo husika.
Tunawaomba wabunge husika waje kuyachukua kabla ya Agosti 30, vinginevyo
tutaziomba mamlaka husika ziyagawe kwenye maeneo yenye mahitaji,” alisema.
Dk Mwinyi aliyataja majimbo na mikoa
ambayo hadi sasa hayajachukua madawati hayo kuwa ni Tanga katika majimbo ya
Kilindi na Pangani (1,611) na Njombe majimbo ya Makambako, Ludewa, Wanging’ombe
na Makete (2,148).
Maeneo mengine ni Iringa katika
majimbo ya Iringa Mjini, Mbeya Mjini na Mbeya Vijijini (91,611), Ruvuma Jimbo
la Tunduru Kaskazini ( 537) na Mbeya katika majimbo ya Ileje, Kyela, Rungwe na
Busokelo ( 2,148).
Mengine ni Songwe ( 537) na Kwela,
Nkasi Kaskazini na Nkasi Kusini (Rukwa) (1,611). Kwa mujibu wa Dk Mwinyi,
kutochukuliwa kwa madawati hayo kunasababisha kukosekana kwa nafasi ya kuweka
madawati mengine yanayotengenezwa kwenye vituo mbalimbali vya JKT.
Pia, alisema yanapoendelea kubaki
mahali hapo yanapigwa jua, kunyeshwa na kupungua ubora. Pamoja na hayo, alisema
kuwa awamu ya pili ya madawati 30,000 inaendelea vyema kwa kuwa tayari madawati
20,000 yamekamilika na yanaweza kuchukuliwa na kugawanywa panapohusika.
Alisema, “madawati 10,000 yaliyobaki
yatakamilika kabla ya Oktoba 30,000 kama ilivyopangwa na yatagawanywa katika
majimbo 51”.
Aprili 11, mwaka huu, Bunge
lilimkabidhi Dk Magufuli Sh bilioni sita ilizoziokoa kwa kubana matumizi katika
maeneo mbalimbali kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, ikiwemo posho, safari
za nje na viburudisho, ambazo Rais aliagiza zitumike kununua madawati kwa kila
jimbo.
No comments:
Post a Comment