Waziri
wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba amewasili mkoa wa Geita kwa ziara ya
kikazi, kubwa ikiwa ni kufuatia taarifa za mateso na mauaji yaliyodaiwa
kufanywa na raia wa China wanaomiliki sehemu ya mgodi wa Nyamhuna uliopo
Katoro, Geita dhidi ya wafanyakazi/vibarua ambao ni Watanzania.
Takribani wiki moja sasa kumekuwa na hali ya sintofahamu dhidi ya picha zinazoenezwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari zikionesha raia wa Tanzania anayefanya kazi kwenye mgodi tajwa akiteswa na kufanyiwa vitendo ya kinyama na mwajili wake ambaye ni raia wa china.Ilimlazimu Waziri mwenye dhamana na usalama wa raia na mali zao kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kufika eneo la mgodi kujiridhisha kwa taarifa zilizotapakaa na kubeba simanzi kwa Watanzania.
Mwigulu Nchemba amejiridhisha kuwa
kulikuwepo na tukio hilo la Mtanzania kuteswa na mwajiri wake, kipigo
kilichosababisha kupoteza fahamu na siyo kifo.Hatua za awali Waziri Nchemba
alizozifanya ni kwenda gereza la Geita mjini alikohifadhiwa kijana huyo kwa
madai ya kushitakiwa na mwajiri wake kwa kosa la wizi lililosababishwa apigwe.
Katika mahojiano ya Waziri Mwigulu
Nchemba na kijana huyo, Mwigulu alibaini kuwa kijana huyo aliyepo gerezani
ndiye mhusika hasa wa tukio lile kwa uthibitisho wa makovu yaliyopo mwili mwake
na mavazi aliyovalia wakati anateswa na akiwapo gerezani.
Katika hali hiyo, ilimlazimu, Mhe.
Mwigulu kwenda mgodini akiwa ameambatana na kijana huyo kwa ajili ya kutambua
waliofanya vitendo hivyo vya kinyama.
Katika oparesheni hiyo, kijana
aliyeteswa na kujeruhiwa aliwabaini Watanzania 5 ambao ni walinzi wa eneo hilo
na Mchina mmoja walioshirikiana kumpiga, kumtesa na kumjeruhi.Kufuatia utambuzi
huo na maelezo ya wahusika, Nchemba akaagiza wahusika wakamatwe mara moja na
akaondoka nao kwa hatua zaidi za kisheria.
Katika hali nyingine ya kusikitisha,
Waziri Nchemba amebaini uwepo wa wahamiaji haramu raia wa China katika mgodi
huo ambapo nyaraka za uhamiaji mkoa wa Geita zinaonesha raia 28 wenye vibali
ndio waliruhusiwa kukaa kwenye mgodi huo, lakini katika operasheni ya
kushitukiza aliyoifanya Mhe. Nchemba amebaini uwepo wa raia wa china zaidi ya
50 wanaoishi katika mgodi huo kinyume na sheria.
Hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa na
timu yake ya uhamiaji kuhakikisha wote wasio na vibali wanakamatwa na
kuchukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment