
KLABU
Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo imeachana rasmi na aliyekuwa
Kocha Mkuu wake, Stewart Hall, baada ya kufanyika makubaliano ya pande zote
mbili.Uongozi
wa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, umechukua hatua hiyo kufuatia hivi
karibuni Hall kutangaza uamuzi wa kuachia ngazi akiweka wazi kuwa amechoka
kufundisha soka Tanzania na sasa anataka kwenda kutafuta changamoto nyingine
mpya ya kufundisha soka nje ya nchi.
Akizungumza na mtandao
rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema mara baada ya kukaa meza moja na Hall
wamekubaliana kwa pamoja juu ya ombi lake hilo huku akieleza kuwa kwa sasa
kikosi hicho kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi Dennis Kitambi.
Alisema Kitambi
atakinoa kikosi hicho katika mechi mbili zilizobakia msimu huu, ya Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mgambo JKT itakayofanyika Jumapili hii
(Mei 22) pamoja na ile ya fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports
Federation Cup) watakayokipiga na Yanga Juni 11 mwaka huu.
“Leo tumeachana na Hall
kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya kutuomba kuachia ngazi kwa lengo
la kutafuta changamoto nyingine nje ya nchi, wakati tukijipanga kuunda benchi
jipya la ufundi kwa sasa timu itakuwa chini ya Kocha Msaidizi Dennis Kitambi
hadi kumalizika kwa msimu huu,” alisema.
Kawemba pia alichukua
fursa hiyo kumpongeza Hall kwa mafanikio aliyoipa timu hiyo kwa muda mchache
aliofanya kazi ndani ya Azam FC huku akimtakia kila la kheri katika timu
nyingine atakayokwenda kuifundisha.
“Tunamshukuru Hall kwa
mafanikio aliyotupa msimu huu, kwanza kutupa ubingwa wa Kombe la Kagame,
kuingia fainali ya Kombe la FA na sasa tukiwa nafasi ya pili kwenye ligi, hii
ni rekodi nzuri na tunamshukuru sana kwa hilo na tunapenda kumtakia kila la kheri
katika timu nyingine atakayokwenda kufundisha,” alisema.
Rekodi ya Hall Azam FC
Kocha huyo raia ya
Uingereza aliyeifundisha Azam FC kwa nyakati tatu tofauti, tokea aanze kibarua
hicho Juni mwaka jana anaondoka akiwa ameinoa timu hiyo katika jumla ya mechi
62 msimu huu, akishinda mara 41, sare 16 na kufungwa mechi tano.Katika idadi
hiyo ya mechi, Hall ameiongoza Azam FC kufunga jumla ya mabao 111 na kufungwa
41, huku akimaliza mechi bila kufungwa bao lolote (cleensheet) ndani ya michezo
31 pekee.
No comments:
Post a Comment