MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya DRC,
Thomas Ulimwengu amesema kwamba hafurahii maisha katika klabu yake hiyo na sasa
anataka kuondoka, lakini kila ofa inayokuja ‘inatiwa kapuni’.
Akizungumza
na vyombo vya habari Ulimwengu, mshambuliaji mwenye nguvu,
kasi na uwezo mkubwa wa kuwapita mabeki, alisema kwamba mmiliki wa klabu yao,
Moise Katumbi Chapwe amekuwa akiwabania kuondoka.
“Inaniuma
sana hadi sasa bado nacheza Afrika, zinakuja ofa nyingi tunatakiwa na klabu za
Ulaya, lakini bosi anakataa, kisa bado tuna Mkataba na timu,”amesema Ulimwengu.
Mshambuliaji
huyo wa zamani wa Moro United, amesema kwamba anapojaribu kwenda kumuulizia
bosi wake huyo juu ya ofa hiyo amekuwa kama ‘akipotezea’.
Kuna
wakati baada ya kusemea hajapata ofa ya klabu moja ambayo nilikuwa nina uhakika
imefika, ikabidi niwaambie wale jamaa wanitumie mimi nimpelekee yeye mkono kwa
mkono, lakini pamoja na kufanya hivyo, bado alizungua,”amesema Ulimwengu.
Mshambuliaji
huyo tegemeo wa Tanzania kwa sasa amesema kwamba kwa sasa anasubiri tu kumaliza
Mkataba wake mwakani, ili aangalie ustaarabu mwingine.
Lakini
Ulimwengu amesema inamuuma sana katika wakati huu ambao klabu nyingi za Ulaya
zinamtaka, Mazembe inambania.
“Yaani
imefika wakati sikufichi ndugu yangu, nafurahi tu kwa sababu pale nakubalika,
nina marafiki, mashabiki wananikubali, lakini nikifikiria kwamba napoteza
nafasi za kusogea mbele, nakosa furaha kabisa,”amesema.
Pamoja
na hayo, Ulimwengu amesema hakati tamaa, ataendelea kuitumikia Mazembe kwa
uadilifu wa hali ya juu hadi hapo atakapomaliza Mkataba wake aondoke salama.

No comments:
Post a Comment