Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Februari, 2015
umeongezeka kwa asilimia 4.2 kutoka asilimia 4.0 mwezi Januari
mwaka 2015.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu
za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambapo amesema
kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi
Februari, 2015 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka
ulioishia mwezi Januari, 2015.
“Kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari,
2015 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na
bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Februari, 2015
zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014, amesema Kwesigabo”.
Bidhaa za vyakula zilizoonyesha kuongezeka mwezi
Februari, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014 ni pamoja na bei
za mchele (asilimia 18.5), unga wa mihogo (asilimia 9.3), nyama (asilimia 8.9),
samaki (asilimia 12.4) na maharagwe kwa asilimia 7.1.
Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoonyesha
kuongezeka mwezi Februari, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014
ni pamoja na bei za mavazi ya wanaume (asilimia 4.7), mavazi ya wanawake
(asilimia 3.3), mkaa (asilimia 5.1), mashuka (asilimia 3.1) na gharama za kumuona
daktari kwa asilimia 11.2.
Akizungumzia kuhusu Mfumuko wa Bei kwa kipimo cha
mwezi Mkurugenzi Kwesigabo amesema kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari, 2015
unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 1.6 ukilinganisha na
ongezeko la asilimia 1.0 mwezi Januari, 2015.
Aidha, Kwesigabo amesisitiza kuwa Fahirisi za Bei
zimeongezeka hadi kufikia 154.83 mwezi Februari, 2015 kutoka 152.43 mwezi
Januari, 2015 ambapo kuongezeka kwa fahirisi kumechangiwa na kuongezeka kwa bei
za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.
Kwa upande wa thamani ya shilingi, Mkurugenzi wa
Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo amesema uwezo wa Shilingi 100 ya
Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 64 na senti 59 mwezi
Februari, 2015 kutoka mwezi Septemba, 2010 ikilinganishwa na Shilingi 65 na
senti 60 ilivyokuwa mwezi Januari, 2015.
Hata hivyo, Mfumuko wa Bei nchini Tanzania una
mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa kuwa
Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari, 2015 nchini Uganda umeongezeka hadi asilimia
1.4 kutoka asilimia 1.3 mwezi Januari, 2015; na nchini Kenya, Mfumuko wa Bei wa
Mwezi Februari, 2015 umeongezeka hadi asilimia 5.61 kutoka asilimia 5.53 mwezi
Januari, 2015.
No comments:
Post a Comment