CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kimesema hakitaunda tena Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya
kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kutokana na baadhi ya washiriki wake
kuvuruga utaratibu na misingi ya kuanzishwa kwa serikali hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu
wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi
Zanzibar, Waride Bakari Jabu wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika
Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa jana.
Waride alisema makubaliano
yanayotokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sasa yameanza
kuvurugwa na kukiukwa kidogo kidogo katika misingi yake mikuu huku kauli za
chuki na uhasama zikitawala.
Alikumbusha viongozi wa vyama
vya siasa kwamba sababu za kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni tofauti
za kisiasa na kauli za chuki ambazo zilisababisha kuwepo kwa malumbano ya
kisiasa katika majukwaa ya kisiasa.
Alisema kwa bahati mbaya,
misingi hiyo sasa imeanza kuyumba na kuporomoka kidogo huku matusi na kejeli
kwa viongozi wakuu wa serikali akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein,
zikichukua nafasi kubwa.
“Chama Cha Mapinduzi
kimesikitishwa sana na kauli za chuki na uhasama, zinazotolewa na Makamo wa
Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad ambazo zinaashiria kuyumba kwa serikali
ya umoja wa kitaifa na kurudisha chuki na uhasama,” alisema.
Waride alifafanua kwamba CCM
ambayo ni mshirika anayeunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inatamka bayana
kwamba haipo tayari kushiriki kuunda serikali hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka huu.
Alifahamisha CCM haikuwa na
sababu ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu ilipata ushindi wa
kutosha, uliowafanya kuunda serikali. Hata hivyo ilifanya hivyo kwa ajili ya
kukidhi matakwa ya sheria.
“CCM haioni sababu tena ya
kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa sababu wenzetu CUF wamekuwa wakitoa
kauli za chuki na uhasama zinazorudisha nyuma matarajio ya wananchi wa kuwepo
maridhiano ya kisiasa,” alisema.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa
iliundwa kisheria mwaka 2010 baada ya vyama vikuu vya siasa visiwani hapa, CCM
na CUF, kujadiliana na hatimaye kufikia mwafaka wa kugawana madaraka, kuondoa
siasa za chuki, zilizotokana na machafuko ya mwaka 2005 wakati wananchi
walipokuwa wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais.
Katika hatua nyingine, Kamati
Kuu ya CCM itakutana Jumamosi ijayo kujadili mambo mbalimbali. Taarifa
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa vikao vingine muhimu vya
chama hicho, vinaendelea kufanyika kwa ajili ya kikao hicho cha juu.
Chanzo Habari Leo
No comments:
Post a Comment