1.
Mbwa mwenye mnofu mdomoni hapigi kelele (Kifipa) Maana yake ni kama methali ya kiswahili
isemayo:- Mwenye shibe hamjui mwenye njaa. Methali hii hutumiwa kwa kuwasema
watu ambao wana kitu na huwasahau wale ambao hawana kitu. Zaidi, huweza
kutumika kwa kuwaonya viongozi wanaosahau kuwatetea wenzao baada ya kupata
madaraka na shibe.
2. Acha kukuna makovu ya mende (Kichaga)
Maana yake ni kwamba uache kukumbuka taabu ya wakati uliopita. Methali hii itafahamika vizuri kama tukielewa kwamba hapo zamani katika jamii zetu, mende walikuwa wanaonekana kwa wingi katika nyumba. Nao mende ni hodari wa kuuma watu wakati wa usiku wakiwa wamelala. Na pale walipouma hubaki kovu ambalo hukuna. Lakini pia ambaye ameshaumwa na mende hao itakuwa ni kazi bure kama atakalia kuyakuna makovu hayo.
Methali hii hutumika kwa kuwaonya watu wasikalie kufikiria makosa au taabu za wakati uliopita.
3. Afadhali kuchakaza nguo kuliko akili (Kipare)
Maana yake ni kuwa hakuna kitu bora kama akili (hekima). Mtu ambaye hana hekima ya uchi kuliko uchi wa aina yoyote ile. Kuwa uchi kinguo, mtu anaweza kununua zingine. Lakini mtu anapokuwa uchi kiakili, hakuna maarifa.
Methali hii hutumika kwa kumhurumia mtu ambaye ameharibikiwa na akili na anafanya majambo isivyotakiwa katika jamii.
4. Amekufa hata Mwakafwile aliacha mwana alipokufa (Kinyakyusa)
Methali hii inatokana na mila za kibantu kukosa mrithi ni mwisho wa ukoo na jina la ukoo. Mtoto wa kiume huendeleza ukoo. Ni jambo la kusikitisha sana kutokuwa na mwana mrithi.
Maana ya methali hii ni kwamba mtu anayehusika hana msaada wowote kutoka kwa ndugu, jirani au mahali penginepo.
Hutumika na mtu binafsi aliyezama ndani ya kilindi kikubwa cha matatizo, wala hana mtoto au mtu wa karibu naye ambaye angeweza kumsaidia. Ni methali ya watu maskini na wanyonge katika kuhurumiana shidani. Kama kuunguliwa nyumba, kufiwa nk.
No comments:
Post a Comment