VAN GAAL ACHUKIZWA NA RATIBA YA LIGI KUU KIPINDI CHA KRISMASI.
MENEJA wa klabu ya Manchester
United, Louis van Gaal ameonyesha kutofurahishwa na ratiba ya Ligi Kuu
itakavyokuwa katika kipindi cha sikukuu za krismasi na mwaka mpya. Kuna
uwezekano mkubwa United ikacheza mechi nne ndani ya siku tisa katika kipindi
cha kati ya Desemba 29 mpaka Januari 3 kutegemeana na ratiba ya Kombe la FA
itakavyokuwa. Ratiba katika Ligi Kuu inaonyesha kuwa watakuwa wenyeji wa
Newcastle United Desemba 26, kabla ya kucheza wa ugenini dhidi ya tottenham
Hotspurs siku mbili baadae na siku ya mwaka mpya watapepetana na Stoke City.
Akihojiwa Van Gaal amesema ana mke, watoto na wajukuu na hawezi kuwaona katika
kipindi cha krismasi lakini alitaka kufanya kazi katika Ligi Kuu hivyo anapaswa
kuzoea hali iliyopo. Van Gaal amesema hafurahishwi na suala hilo lakini hawezi
kubadilisha na hadhani kama ni jambo zuri kwa wachezaji pia.
GRANT KUANIKA MIPANGO GHANA JUMATANO.
KOCHA mpya wa timu ya taifa ya
Ghana, Avram Grant ameanza kazi rasmi leo huku akitegemewa kuweka mikakati yake
katikati ya wiki. Jumatano kocha huyo wa zamani wa Chelsea raia wa Israel
anatarajiwa kuzungumza na wanahabari ili kuweka maono na mipango yake kwa soka
la Ghana. Mkataba rasmi wa kocha huyo unaanza kufanya kazi leo lakini Chama cha
Soka cha Ghana kimethibitisha kuwa tayari kocha huyo ameshatua na ataanza rasmi
kibarua chake hicho kesho. Moja ya kibarua atakachokuwa nacho Grant mwenye umri
wa miaka 59 ni kusaidia kujenga shule ya soka ya kitaifa na pia kusaidia
mafunzo ya makocha wazawa wan chi hiyo. Grant ana wiki sita za kukiandaa kikosi
kipya cha Ghana kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika huko
Guinea ya Ikweta mapema mwakani
SHABIKI MMOJA AFARIKI KATIKA VURUGU HISPANIA KABLA YA MCHEZO WA
ATLETICO NA DEPORTIVO.
SHABIKI mmoja amefariki dunia baada
ya vurugu kati ya mashabiki kabla ya mchezo wa La Liga kati ya Atletico Madrid
dhidi ya Deportivo La Coruna jana. Shabiki huyo wa Deportivo anayekadiriwa kuwa
na umri wa miaka 43 aliondolewa katika mto karibu na Uwanja wa Vincente Calderon
unaomilikiwa na Atletico akiwa amepatwa na mshituko wa moyo, baridi yabisi na
majeraha ya kichwani na kufia hospitalini. Watu saba wangine walitibiwa
majeraha madogo madogo akiwemo polisi mwanamke kutokana na vurugu hizo. Watu 20
walikamatwa na polisi huku wengine 100 walioanzisha vurugu hizo nao
wakitambuliwa. Vurugu hizo zimelaaniwa vikali na vilabu vyote viwili pamoja na
maofisa wa La Liga. Baadae katika mchezo huo Atletico walishinda kwa mabao 2-0
ukiwa ni ushindi wao watano mfululizo na kuwasogelea vinara wa La Liga Real
Madrid kwa tofauti ya alama nne.
APPIAH AMTEUA SWAHIBA WAKE KUMSAIDIA KAZI HUKO SUDAN.
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya
Ghana, Kwesi Appiah amemteua rafiki yake wa siku nyingi Prince Owusu kuwa
msaidizi wake katika kibarua chake kipya huko nchini Sudan. Mara baada ya
kuteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Al-Khartoum Appiah aliamua kumvuta Owusu kuwa
msaidizi wake baada ya wawili hao kufanya kazi pamoja kwa kipindi kirefu sasa.
Owusu sio mgeni sana nchini Sudan kwani mara kadhaa amekuwa akiteuliwa kwenda
huko kwa ajili ya mafunzo mafupi ya makocha. Wawili hao wanatarajiwa kusafiri
kuelekea nchini Sudan Desemba 10 mwaka huu tayari kuanza kazi yao hiyo mpya.
Al-Khartoum iko katika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu nchini humo na
wanatarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani.
GERRARD KUPEWA MKATABA MPYA - RODGERS.
MENEJA wa klabu ya Liverpool,
Brendan Rodgers amesema timu hiyo tayari imeshamuofa mkataba mpya kiungo na
nahodha wao Steven Gerrard. Kocha huyo pia alikanusha tetesi za kutoelewana na
Gerrard ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu
huu. Akizungumza kabla ya mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Leicester,
Rodgers amesema hakuna ugomvi wowote kati yake na Gerrard na kudai hayo
yanayosemwa hayana ukweli wowote. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa Gerrard
atapewa muda wa kufikiria ofa hiyo mpya lakini amedai pesa haitakuwa tatizo.
Rodgers amesema amekuwa akifurahia kila dakika kufanya kazi na Gerrard na ni
matumaini yake ataendelea kuitumikia klabu hiyo.
ENRIQUE AKEMEA VURUGU ZA MASHABIKI BAADA YA MESSI KUPIGWA CHUPA.
MENEJA wa klabu ya Barcelona, Luis
Enrique amesema vilabu nchini Hispania vinapambana dhidi ya mashabiki
wanaojaribu kufanya vurugu wakati wa mechi. Kauli hiyo ya Enrique imekuja
kufuatia Lionel Messi kupigwa na chupa ya plastiki wakati akishangilia ushindi
dhidi ya Valencia katika mchezo wa La Liga uliochezwa jana. Messi hakuumia
katika tukio lakini Enrique amesema kinachotokea ndani ya uwanja kinaweza
kuzuiliwa. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa unaweza kuwa na mtu yeyote ambaye
anatamani kuanzisha vurugu lakini wanapamabna na kupinga matukio hayo.
No comments:
Post a Comment