Dar es Salaam. Mabadiliko
ya wakuu wa mikoa yaliyotangazwa juzi na Rais Jakaya Kikwete yametajwa kuwa na
malengo ya kisiasa, huku Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa akikosoa
kitendo cha kuhamishwa vituo vya kazi wakuu hao sita ndani ya mwezi mmoja,
kwamba ni gharama kwa Serikali.

Wakizungumza
na gazeti hili wasomi nchini wamesema mabadiliko ya wakuu hao huwa na sababu
nyingi, lakini sababu ambayo haielezwi huwa ni ile ya kisiasa.
Katika
mabadiliko hayo Rais Kikwete alimpandisha cheo Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Daudi
Ntibenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kuwahamisha vituo vya kazi wakuu
wengine sita wa mikoa kuanzia juzi. Ntibenda aliapishwa jana Ikulu na Rais
Kikwete.
Uhamisho huo umekuja ikiwa ni mwezi
mmoja kamili tangu Rais Kikwete alipofanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa mikoa
na kuwahamisha sita, huku wengine watatu wakipangiwa kazi nyingine.
Wakuu
wa mikoa wanne wapya ni Dk Ibrahim Msengi (Katavi), Amina Masenza (Iringa),
Halima Dendego (Mtwara) na John Mongella (Kagera).
Akizungumza
na gazeti hili Dk Slaa alisema, “Mabadiliko haya ni viashiria vya Serikali
kuchoka na kutokuwa na uhakika kama itabakia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu
2015. Ndiyo maana wanawahamisha ili kuona nani atafaa wapi na kwa malengo
gani.”
Alisema
kumhamisha mkuu wa mkoa ndani ya mwezi mmoja ni gharama zisizo na msingi, “Hizi
gharama zote za nini? Hivi hawazioni, iweje katika kipindi hiki kifupi wafanye
mabadiliko haya?
“Katika
kipindi hiki ambacho nchi inahitaji fedha kwa ajili ya shughuli nyingi za
maendeleo, yanapofanyika mabadiliko kama haya lazima ujiulize kipaumbele cha
Serikali ni nini,” alisema.
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema: “Binafsi
naona mabadiliko haya yanalenga uchaguzi mkuu maana kila unapokaribia huwa
yanafanyika.”
Mhadhiri
Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander
Makulilo alisema: “Suala la gharama haliepukiki. Sababu za kuhamisha wakuu wa
mikoa ni nyingi ila kubwa ni changamoto za mkoa husika au kupwaya katika
utendaji.”
Hata
hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema mabadiliko hayo ni ya
kawaida na yametokana na kupewa likizo ya ugonjwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Paschal Mabiti ambaye nafasi yake imechukuliwa na Elaston Mbwilo
aliyetoka Manyara.
“Kunapokuwa
na tatizo kama hilo ni lazima Rais ateue watu wengine. Rais anapoteua anatazama
hata changamoto za mkoa husika na uteuzi unazingatia zaidi utendaji si masuala
ya kisiasa. Baadaye utafanyika uteuzi wa wakuu wa wilaya,” alisema.
Katika
uteuzi huo wa juzi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera anahamia Manyara
kutoka Morogoro na nafasi yake inachukuliwa na Dk Rajabu Rutengwe kutoka Tanga
alikokaa kwa mwezi mmoja akitokea Katavi.
Magalula
Magalula amehamishiwa Tanga kutoka Lindi ambako naye alikaa kwa mwezi mmoja
akitokea Geita na nafasi yake inazibwa na Mwantumu Mahiza kutoka Pwani.
Mhandisi Evarist Ndiliko amehamishiwa Mkoa wa Pwani kutoka Arusha alikohamia
hivi karibuni akitokea Mwanza. Walioachwa kwa ajili ya kazi nyingine ni Dk
Christine Ishengoma (Iringa), Kanali Fabian Massawe (Kagera) na Kanali Joseph
Simbakalia.
.aliyekuwa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ambaye tayari ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).
Akizungumza
Ikulu jana mara baada ya kuapishwa, Ntibenda alisema, “Siendi Arusha kupambana
na vurugu, ninakwenda kusimamia masuala ya maendeleo.”
Alisema
changamoto zinazoukabili mkoa huo ni migogoro ya ardhi na kusisitiza kuwa
ataitatua migogoro hiyo kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wakuu wa mikoa.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment