WATU 13 wamekufa na wengine zaidi ya 19
kujeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarani, iliyohusisha basi dogo la abiria
aina ya Toyota Double Coaster, linalosafiri kati ya mjini Tanga na Lushoto,
kugongana na lori la mizigo aina ya Scania, lililokuwa likitokea Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, ajali hiyo
ilitokea juzi eneo la Mkanyageni saa moja asubuhi wakati magari hayo yalipokuwa
yanapishana.
Alisema
ajali hiyo, ilihusisha basi dogo lenye namba za usajili T 410 BJD lililokuwa
likiendeshwa na Bakari Musa na lori lenye namba za usajili T 645 LBJ likiwa na
tela lenye namba T 605 ABJ, lililokuwa likiendeshwa na Benjamin Abeid.
Alisema
chanzo cha ajali hiyo ni lori hilo, lililokuwa likitokea upande wa Dar es
Salaam kwenda Tanga, ambapo baada ya kufika eneo la tukio lilizidi upande wa
kulia na kuligonga basi hilo la abiria na kusababisha ajali.
Akizungumzia
ajali hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Aisha Mahita alisema maiti na
majeruhi wa ajali hiyo, wamepelekwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza.
Dk
Mahita alisema majeruhi waliopokelewa hospitalini hapo ni 25, ambapo kati yao
19 ni wanaume na 6 ni wanawake.
“Majeruhi
baadhi wamepata vidonda na wengine wamevunjika mikononi na miguu, lakini
wanaendelea kupatiwa matibabu hapo teule huku majeruhi wawili kati ya hao
wakiwa wamelazwa kwenye chumba cha uangalizi maalum (ICU),” alisema.
Kuhusu
abiria waliopoteza maisha katika ajali hiyo, Dk Mahita alisema kati yao wanaume
ni saba na wanawake ni watano, ambapo tayari maiti saba wameweza kutambuliwa na
ndugu zao.
Kutokana
na ajali hiyo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa
wa Tanga, Dk Rajabu Rutengwe kuomboleza vifo vya abiria hao, akisema:
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kupotea ghafla kwa maisha ya watu
13 na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea katika
Mkoa wako wa Tanga”.
Rais
Kikwete alisema “Naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo
wangu kutokana na vifo hivyo, na kupitia kwako, naomba salamu za pole ziwafikie
watu wote waliopotelewa na ndugu na jamaa zao kwenye ajali hiyo”.
Alisema
anawaomba wote waliopoteza ndugu na jamaa zao kwenye ajali hiyo, wawe watulivu na
wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, na aliwahakikishia kuwa
yuko pamoja nao katika kipindi chote cha maombolezo.
“Kwa
wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo, namwomba Mungu awajalie ahueni na wapone
haraka, ili warejee tena katika hali zao za kawaida. Namwomba Mola azipokee na
kuzilaza mahala pema peponi Roho za Marehemu wote, Amina”, alisema Rais
Kikwete.
No comments:
Post a Comment