BARAZA la Sanaa la
Taifa (BASATA), limesema kwamba linaendelea na uchunguzi kuhusu sakata la
ushindi wa mrembo wa Tanzania 2014, Sitti Mtemvu na wiki hii litakutana na
mwandaaji wa shindano hilo, Hashim Lundenga.
Sitti ameingia katika mzozo na mamlaka za
Serikali baada ya kudaiwa kukiuka kanuni za uendeshaji wa mashindano hayo kwa
kuwasilisha cheti kinachoonesha umri ulio kinyume cha umri wake halali, jambo
ambalo kwa mujibu wa taratibu za mashindano hayo, hakupaswa kushiriki.
Mshindi huyo wa kitongoji cha Chang’ombe na
kisha Kanda ya Temeke, anadaiwa kughushi cheti kipya cha kuzaliwa kilichotolewa
Septemba mwaka huu kinachoonesha kuwa alizaliwa mwaka 1991, badala ya kile cha
awali ambacho kinaoonesha alizaliwa Mei 31, 1989, umri wake sahihi unaomfanya
awe na miaka 25.
Redd's Miss
Temeke 2014, Sitti Mtemvu akipunga mkono huku akiwa na mshindi wa Pili, Salma
Saleh (kushoto) na watatu, Neema Mollel, baada ya kutangazwa kuwa washindi wa
shindano hilo.
|
Kwa mujibu wa taratibu za Kamati ya Miss
Tanzania, warembo wanaoshiriki shindano hilo hawapaswi kuzidi umri wa miaka 23,
umri ambao tayari kwa mujibu wa vielelezo kadhaa umevukwa na Sitti.
Akizungumza jana kwa simu na gazeti la Habari Leo ,
Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Lebejo alisema wanaendelea na
uchunguzi wa sakata hilo na kwamba wiki hii watakutana na Lundenga.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Lebejo |
Wakati Basata ikieleza hayo, habari zinadai
kuwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), wamekwisha kukifuta cheti
kinachotangazwa kupatiwa Sitti, Septemba mwaka huu, kwani si halali kwa mujibu wa
vielelezo vyao.
Inadaiwa kuwa Rita baada ya kufikia uamuzi
huo, imeiarifu Basata ikiitaka ichukue hatua stahiki kwa mrembo huyo ikiwamo
kumvua taji hilo, lakini Lebejo alisema jana kuwa wao kama hilo lipo hivyo ni
la Rita, kwa sababu wao hawashughuliki na vyeti, bali wakala hao.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment