KAMPUNI YA PAP YASEMA HAINA UHUSIANO WA UMILIKI NA FAMILIA YA RAIS KIKWETE.
KAMPUNI ya Pan Africa Power Resources (PAP) imesema haina mahusiano ya
kiumiliki na familia ya Rais Jakaya Kikwete, kama umma unavyoaminishwa kwa
kuwekewa taarifa sizizo za kweli kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Taarifa ya kupinga tuhuma hizo ilitolewa jana na Katibu na Mshauri Mkuu wa
Sheria wa Kampuni ya IPTL inayomilikiwa na PAP, Joseph Makandege, alipozungumza
na waandishi wa habari.
Hivi karibuni mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, aitwaye Miraji alisikitishwa na tuhuma
hizo zinazotolewa dhidi yake kuhusishwa na umiliki wa kampuni ya PAP kwamba
yeye na dada yake, Salama wanamiliki asilimia 50 za PAP kupitia Simba Trust,
wakati si kweli.
Akizungumzia jambo hilo, Makandege alisema PAP inamilikiwa kwa asilimia 50 na
Harbidher Sing Seth na Simba Trust, ambayo nayo inamiliki asilimia 50.
Kwa mujibu wa Makandege alisema majina ya wamiliki wa Simba Trust ni Settler
Clive Anthony Cooke, Pamela Sethi na Hardeep Kaur Chaggar.
Alisema hakuna sehemu yoyote inayoonesha kuwa kuna majina yatokanayo na familia
ya Rais Kikwete, wakiwemo watoto wake, ambao ni Salama na Miraji Kikwete, hivyo
huo ni mwendelezo wa upotoshaji wa uongo unaofanywa na wanasiasa na baadhi ya
watu juu ya IPTL.
“Taarifa zinazosambazwa katika mitandao zina lengo la kuichafua familia ya Rais
Kikwete na IPTL na ndio maana tumeona tufafanue ukweli halisi wa jambo hili ili
umma uelewe,”alisema.
Makandege alisema PAP/IPTL haipendi kuzungumza na vyombo vya habari kuhusiana
na sakata la ESCROW linaloendelea bungeni kwa kuwa wanasubiri ripoti ya
serikali.
“Tunasubiri ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na
Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG),”alisema.
Hivyo, Makandege aliwataka Watanzania kuwa makini na taarifa zinazosambazwa
katika mitandao kwa kuwa hazielezi ukweli wa jambo hilo
No comments:
Post a Comment