MKAZI wa
Kijiji cha Vikonge, Kata ya Mpandandogo wilayani Mpanda, Joseph Lukato (52)
amejinyonga kwa kujitundika mtini akitumia mtandio wa mkewe baada ya
kughadhabika na kuachwa naye.
Kaimu Kamanda
wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Focas Malengo, alisema tukio hilo lilitokea
Julai 27, mwaka huu saa mbili asubuhi kijijini hapo ambapo alijinyonga katika
shamba la jirani yake.
Kamanda huyo
alisema Lukato alikuwa na ugomvi wa muda mrefu na mkewe Mary Joseph (42)
aliyekuwa akimtuhumu kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanaume mwingine kijijini
hapo.
Alisema siku
ya Julai 19, mwaka huu, Lukato alirejea nyumbani kwake saa nane mchana akitokea
shambani na kula chakula ambapo alimlalamikia mkewe kuwa kilikuwa kibichi.
Alisema hatua
hiyo ilizua ugomvi baina ya wanandoa hao ambapo Lukato alimwambia mkewe kwamba
amempikia chakula kibichi kwa kuwa alichelewa kurudi nyumbani kutoka mwanaume
huyo mwenye uhusiano naye wa kimapenzi.
Kamanda
Malengo alisema mke wa Lukato alijitahidi kujijitetea kwa mumewe kuwa hakuwa
ametoka nyumbani kwake siku hiyo na kumhakikishia mumewe kuwa chakula kilikuwa
kimeiva.
Inadaiwa
Lukato hakukubaliana na utetezi wa mkewe na aliendelea kumshutumu na baadaye
akaanza kumpiga katika ugomvi uliochukua muda mrefu hatua iliyomfanya mke wa
Lukato kurudi nyumbani kwa wazazi wake kwa kuhofia usalama wa maisha yake.
“Lukato
alijitahidi kufanya jitihada za mara kwa mara za kumshawishi mkewe arudi
nyumbani kwake ili wakaendelee kuishi kama walivyokuwa wakiishi awali lakini
mkewe alikataa kurejea, hatua iliyomfanya Lukato kujinyonga,” alisema Kamanda.
Alisema mwili
wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kidaktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu
wa marehemu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
No comments:
Post a Comment