Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni John Mnyika akizungumza Bungeni Mjini Dodoma(Picha na Maktaba) |
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
imeilipua Serikali kwa kushindwa kudhibiti utoroshwaji mkubwa wa fedha kwenda
nje.
Msemaji wa kambi hiyo, John Mnyika
alisema katika kipindi cha miaka 39 kuanzia 1970 hadi 2008, Sh9.6 trilioni
zilitoroshwa kiharamu kwenda nje.
"Utoroshaji wa fedha hizi
unasadikiwa kutokana na ukwepaji wa kodi, na misamaha mikubwa ya kodi,"
alisema Mnyika na kuongeza; "Fedha nyingine zilitokana na usiri mkubwa wa
mikataba baina ya wawekezaji na Serikali, upotoshaji wa bei katika biashara na
rushwa katika mikataba na wawekezaji" alisema.(P.T)
Mnyika alisema Serikali ya CCM haiwezi
kukwepa kuwajibika kwa sababu utoroshaji wa mapesa yote haya umefanyika wakati
na CCM ipo madarakani, " alisema.
Mnyika alifafanua, utoroshaji huo wa
fedha ulifanyika kwa mafungu na kutolea mfano mwaka 1980, Dola 570. 6 milioni
zilitoroshwa.
Fedha hizo zilitoroshwa wakati hayati
baba wa Taifa mwalimu Jullius Nyerere akiwa madarakani na dola 1,566 milioni
zikatoroshwa 1985 wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi.
"Jambo la kusikitisha zaidi mwaka
2002 zilitoroshwa jumla ya Dola za Marekani 1,1010 milioni katika kipindi
ambacho Rais Benjamin Mkapa yuko madarakani," alisema Mnyika.
Mnyika alisema kambi hiyo
imesikitishwa na kitendo cha Bunge kushindwa kuisimamia kikamilifu Serikali
hususan Wizara ya Nishati na Madini.
Alisema fedha zote zilizotoroshwa
nchini tangu mwaka 1970 mpaka 2008 zinaweza kurejeshwa nchini kwa kuanzia na
kuzibaini zilipo.
"Uchunguzi wa kina ufanyike
kuzuia fedha hizo katika akaunti za benki zilipotunzwa nje ya nchi na hatimaye
kurejesha fedha hizo nchini," alisema.
Kitengo cha Financial Intelligence
Unit (FIU) cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kimetakiwa kukusanya taarifa za kiintelijensia
na kuziwasilisha Takukuru ili uchunguzi ufanyike.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment