![]() |
| SHUJAA NADIR HARROUB "CANNAVARO" |
BAO pekee
la Nahodha Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ jioni hii limeipa ushindi wa 1-0 Yanga
SC katika mchezo wa kwanza wa kuwania kucheza Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa
Afrika, dhidi ya Al Ahly ya Misri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Cannavaro
alifunga bao hilo dakika ya 87 akimalizia kona maridadi ya winga Simon Msuva
kutoka wingi ya kulia.
Kona hiyo
ilitokana na kipa Sherif Ekram Ahmed kupangua shuti kali la mshambuliaji
Mganda, Emmanuel Okwi.
Katika
mchezo huo uliochezeshwa na refa Heileyesus Bazeze aliyesaidiwa na Kindie
Mussie Tdedesse Shawangiza wote kutoka Ethiopia, hadi mapumziko milango
ilikuwa migumu.
Yanga SC
ndiyo waliotawala zaidi mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa nzuri za kufunga,
lakini wakakosa umakini katika kumalizia.
Simon Msuva
alikuwa chanzo kizuri cha mashambulizi ya Yanga upande wa kulia, lakini Waganda
Emannuel Okwi na Hamisi Kiiza walishindwa kutumia nafasi.
Haruna
Niyonzima, Frank Domayo na Mrisho Ngassa kwa pamoja walicheza vizuri katika
safu ya kiungo kipindi cha kwanza.
Kipindi
cha pili, Ahly kidogo walibadilika na kuongeza kasi ya mashambulizi kupitia kwa
Amr Gamal, ambaye hata hivyo alidhibitiwa vikali na walinzi wa Yanga, ambao leo
walicheza kwa umakini wa hali ya juu.
Mabadiliko
yaliyofanywa na kocha Mholanzi Hans van der Pluijm, kumuingiza mshambuliaji
Didier Kavumbangu kuchukua nafasi ya Hamisi Kiiza yalifufua makali ya safu ya
ushambuliaji ya timu hiyo.
Kavumbangu
aliwapa wakati mgumu mno mabeki wa Ahly tangu alipoingia dakika ya 66 hata
mashabiki wa Yanga wakatamani angekuwa uwanjani tangu mwanzo.
![]() |
| KIKOSI CHA YANGA |
![]() |
| OKWI AKIWAHENYESHA WAARABU LEO |
Pamoja na
kufungwa 1-0, Al Ahly inayofundishwa na kocha Mohamed Yousef, ilionyesha
upinzani kwa Yanga SC, jambo ambalo linaashiria katika mchezo wa marudiano
lolote linaweza kutokea.
Baada ya
matokeo haya, Yanga SC sasa inahitaji sare ya ugenini ili kusonga mbele hatua
ya 16 Bora.
Kihistoria
hii inakuwa mara ya kwanza kabisa Yanga SC inapata ushindi dhidi ya timu ya
Misri na Kaskazini mwa Afrika kwa ujumla, kwani mara zote imekuwa ikifungwa na
kutoa sare.
Kikosi
cha Yanga SC leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima,
Hamisi Kiiza/Didier Kavumbangu dk66, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa/Said
Bahanuzi dk87.
Al Ahly;
Sherif Ekramy Ahmed, Saad El-Din Saad, Mohamed Ghareeb, Ahmed El Moneim, Sayed
Abdel Waheed, Shihab Eldin Saad, Hossam Mohammed, Ramy Abdel Aziz, Moussa
Yedan/Mahmoud Ibrahim dk59, Mohamed Ismail/Ahmed Shakri Abdelraouf dk 73 na
Amri Gamal Sayed/Ahmed Raoud Adam dk88.



No comments:
Post a Comment