Hayati William Mgimwa enzi za Uhai Wake |
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na
huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Mheshimiwa William Mgimwa,
aliyekuwa pia Mbunge wa Jimbo la Kalenga (Mkoa wa Iringa) kupitia Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete amesema
kuwa taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi ambacho taifa linamhitaji
zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake
za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga, mkoani
Iringa.
Kifo cha Mheshimiwa
Mgimwa kimetangazwa mchana wa leo, Jumatano, Januari Mosi, 2014, na Katibu Mkuu
Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Katika tangazo lake,
Balozi Sefue amesema kuwa Waziri Mgimwa ameaga dunia asubuhi ya leo saa 5:20
(Saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic , Pretoria,
Afrika Kusini ambako amekuwa amelazwa kwa muda sasa.
Balozi Sefue amesema
kuwa maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa Waziri Mgimwa yanafanywa na
Serikali kwa kushirikiana na familia yake na kuwa taarifa zaidi za suala hilo
zitatolewa baadaye kwa kadri zinavyopatikana na maandalizi yanavyoendelea.
Katika salamu zake
kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda na kwa familia ya Marehemu Mgimwa,
Rais Kikwete amesema: “Sina maneno ya
kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za kifo cha
Mheshimiwa Mgimwa.
Binafsi nimemtembelea
mara mbili kwenye Hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake
ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia
yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.”
Ameongeza Mheshimiwa
Rais Kikwete: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani
kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu.”
“Napenda kutoa pole
nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana-familia wote kwa kuondokewa na
mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue
kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” amesema
Rais Kikwete.
Rais pia amewatumia
rambirambi wananchi wa Jimbo la Kalenga akisema kuwa wamempoteza mwakilishi na
mtetezi mahiri wa maslahi yao.
Mgimwa aliyezaliwa
January 20, 1950 na kuwa mbunge wa jimbo la Kalenga mkoani Iringa kupitia chama
cha Mapinduzi (CCM)
Dk. Mgimwa alikuwa
mkufunzi katika Chuo cha Benki mkoani Mwanza, kabla ya kufanikiwa kuchaguliwa
kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mkoa wa Iringa, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010.
No comments:
Post a Comment