WAZIRI MKUU Mizengo Pinda |
*Aahidi mabati 780,
mifuko 2,600 ya saruji
kwa walioathirika
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametembelea vijiji vya
Chipogoro na Fufu katika wilaya za Mpwapwa na Chamwino, mkoani Dodoma na
kukagua maeneo mbalimbali ambayo yaliathiriwa na mafuriko kutokana na mvua
kubwa zilizonyesha kati ya Januari 2 hadi Januari 11, mwaka huu.
Akiwa katika kijiji cha Chipogoro tarafa ya Rubi, Waziri
Mkuu alikagua kituo cha polisi na nyumba zilizobomolewa, choo cha zahanati na
kukagua eneo la barabara inayojengwa ya kutoka Dodoma hadi Iringa katika eneo
lenye matatizo ya makaravati kuziba.
Kwenye kijiji cha Fufu katika tarafa ya Makangwa ambacho
kiko umbali wa kilometa 30 kutoka Chipogoro, Waziri Mkuu alikagua maeneo ya
makazi yaliyoathiriwa kwa mafuriko na kukagua baadhi ya nyumba zilizobomoka
kabla ya kuzungumza na wananchi na kuwapa pole.
Akizungumza na wakazi wa vijiji hivyo leo (Ijumaa,
Januari 17, 2014), mara baada ya kupokea taarifa za maafa ya mafuriko hayo,
Waziri Mkuu alimtaka Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Eng. Leonard Chimagu
kuhakikisha anasimamia wakandarasi wa barabara hiyo ambayo ujenzi wake bado
haujakamilika na kuainisha maeneo korofi ili yafanyiwe marekebisho haraka.
“Nimekagua matundu katika daraja moja pale Chipogoro na
kuona ni madogo, mtaalamu anasema uchafu ulioziba ndiyo umesababisha maji
yasipite. Mimi si mhandisi na hizi ni mvua za kwanza tu, sasa yakija maji mengi
zaidi ya haya hali itakuwaje?, alihoji Waziri Mkuu.
“Hata hapa Fufu, kuna mahali nimeona maji yanaonyesha
yalikuja kwa kasi kubwa lakini upenyo wa kuingia kwenye makaravati na kutokea
upande wa pili ni mdogo sana... barabara hii ni mkombozi lakini kama
haitazingatia uhalisia wa maeneo itakuwa ni balaa,” alionya.
Alimtaka pia awasimamie wakandarasi hao ili wanapoweka
matoleo ya maji wahakikishe upande wa pili barabara maji hayo yanakwenda kwenye
mikondo ya mto na siyo kuyaacha tu yasambae kiholela na kuishia kwenye makazi
ya watu au mashamba yao.
Waziri Mkuu aliahidi kutoa mifuko ya saruji 2,600 na
mabati 1,560 ambapo kila kijiji kitapata mifuko 1,300 na mabati 780 ili
kuwasaidia wakazi waliobomolewa nyumba zao waweze kujenga nyumba za kisasa.
Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi
kuwashirikisha wadau wengine katika mkoa huo ili waone wanawezaje kuchangia
upatikanaji wa mabati mengi zaidi kwa ajili ya nyumba zilizoezuliwa.
Kuhusu chakula cha msaada, Waziri Mkuu alimtaka Dk.
Nchimbi aandae makisio ya mahitaji ya chakula yaliyopo na kuyafikisha Ofisi ya
Waziri Mkuu ambako kuna Idara inayosimamia maafa ili waletewe chakula hicho
haraka kwa sababu kipo.
Alisema anakubaliana na ushauri uliotolewa kuhusu suala
la ujenzi wa mabwawa ya kukinga maji ya mvua ili kupunguza kasi ya maji
yanayoporomoka kutoka milimani lakini akasema Serikali imeanza na ujenzi wa
Bwawa la Kidete lililoko wilayani Kilosa tangu yaliyopotokea mafuriko wilayani
humo.
Mapema, akitoa taarifa kwa
Waziri Mkuu, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Alfred Msovella, alisema
nyumba 129 zilibomoka, vyoo 78 vimebomoka kikiwemo cha zahanati ambapo wakazi
1,390 wamepoteza vifaa mbalimbali ikiwemo vyakula, magodoro, vyombo vya ndani
na mifugo.
Bw. Msovella ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa
alisema hivi sasa, wakazi hao wanahitaji mahema 400, magodoro 381, madaftari ya
wanafunzi na dawa za matibabu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Chamwino, Bi. Fatma Salum Ally akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Fufu, alisema
jumla ya nyumba 26 zilibomolewa na mali kama vyakula, samani, vyombo vya
nyumbani na bidhaa za biashara kuharibika.
Alisema eneo la kijiji cha Fufu ni tambarare na liko
chini ya safu za milima na maji ya mvua yanayoporoka kutoka milimani, huondoka
polepole. “Hata hivyo, hali hii ya mafuriko imechochewa na ujenzi wa barabara
kuu kwa kiwango cha lami ambapo tuta la barabara mpya na vidaraja vidogo
vilivyowekwa vimekuwa kizuizi cha maji mengi yanayotoka milimani na hivyo
kuongeza tatizo la mafuriko,” alisema.
Mikutano hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda na
Biashara, Bw. Gregory Teu ambaye pia ni mbunge wa Mpwapwa pamoja na mbunge wa
Mtera, Bw. Livingstone Lusinde.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment