Na Kambi Mbwana Handeni
WANANCHI
na wakazi wa Kata ya Misima, wilayani Handeni mkoani Tanga, wameombwa kutokuwa
na wasiwasi na hatua ya kuingizwa kwenye Halmashauri ya mji kwakuwa mpango huo
sio mbaya kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi.
Hayo
yalisemwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa
Handeni, Thomas Mzinga, alipozungumza na Mtandao wa Handeni Kwetu, juu ya hatua
mbalimbali za kuunganisha eneo hilo na Handeni Mjini.
Alisema
mchakato wote wa kuunganisha mji huo na Kata ya Misima ulifuata sheria zote,
huku akisema woga wa wananchi unatokana na hoja dhaifu kuwa viwanja vyao
vitauzwa na serikali.
“Sio
kweli kama kuingia kwenye Halmashauri ya Mji basi viwanja vyote na mashamba
yaliyokuwapo yatauzwa ovyo na watendaji wa serikali, maana hiyo si sababu ya
kupanua mji wetu.
![]() |
|
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Mji Handeni Thomas Mzinga, akiwa kwenye moja ya matukio ya
kijamii wilayani Handeni, mkoani Tanga.
|
“Wananchi
wameaminishwa uongo ili suala hilo lisiwe na mafanikio, hivyo tunaamini
tutaendelea kuhamasisha wananchi wetu na Watanzania kwa ujumla ili kwenye mambo
ya kimaendeleo tufanye kama inavyopangwa na viongozi wa serikali kwa ujumla
wake,” alisema Mzinga.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo, hatua ya kuunganisha eneo la Misima katika
Halmashauri ya Mji ni kuweka mikakati kabambe ya kuupanua mji wote wa Handeni
na kusogeza pia maendeleo karibu na wananchi.
Kwa
kipindi cha mwaka mmoja sasa, wananchi wa Misima wamekuwa wakivutana na
viongozi wa serikali ya wilaya ya Handeni wakigoma kuingizwa kwenye Halmashauri
ya Mji kwa madai kuwa bado mapema na kijiji hicho kipo mbali kabisa, huku
wakiona kuwa huenda ni mipango ya waheshimiwa hao kusogea karibu ili kuteka
mashamba yao.

No comments:
Post a Comment