Na Oscar Assenga,Korogwe.
JESHI la Polisi mkoani hapa kwa kushirikiana
na wakazi wa Kijiji cha Maili kumi wilayani Korogwe wamefanikiwa kuwakamata
watu saba kwa tuhuma za kuhusika na kuweka mabomu yaliyokuwa yameandaliwa
tayari kwa kulipuka kwenye nyumba mbili tofauti za ibada.
Pamoja na mabomu hao watuhumiwa hao ambao majina
yao yanahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi wanatuhumiwa kuhusika na kukutwa na
vifaa mbalimbali vya kutengenezea milipuko ya mabomu hayo pamoja na silaha za
jadi ambazo pia zilikuwa zimefichwa katika nyumba hizo za ibada huku katika
Kijiji cha Maili kumi wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Watu hao walikamatwa wakiwa na chupa 10 ambapo tano
zilikuwa na Petrol zikiwa na tambi zake ndani,gololi 103 ambazo hutumiwa
kwa milipuko,galoni kubwa mbili zilizokuwa na lita nne za
petrol,majambia,mishale yenye sumu,soksi za kuzuia uso(mask)upinde,Daftari
lenye mafunzo ya kijeshi kuhusu namna kufungua na kufunga silaha.
Vifaa vingine ni mapanga,visu,Mifuko ya Sandarusi
,manati,vifuniko 12 vya maji,kofia nne na vitambaa vya kufunga kichwani pamoja
na Tende walizokuwa wakitumia kama chakula.
Akizungumza katika mahojiano na TANGA RAHA
BLOG ofisini kwake leo,Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Constantine Massawe
alisema kuwa watu hao walikamatwa Disemba 17 mwaka huu majira ya saa 2.00 usiku
huko wilayani Korogwe.
Kamanda Massawe alisema kuwa Askari Polisi wakiwa
kaika kizuizi cha Maili 10 wilaya ya Korogwe waliwatilia shaka vijana watatu wa
kiume waliokuwa wamebeba vifurishi na walipotaka wasimame walikimbilia msituni
na ndipo mmoja alipokamatwa na Askari hao.
“sasa baada ya kukamatwa huyu mmoja na ndipo
alipopekuliwa na kukutwa na vifaa hivyo kwenye begi lake na ndipo msako wa
kuwatafuta hawa wengine ulipoanza”,alisema Kamanda huyo.
Hata hivyo alisema kuwa alisema kuwa katika
msako huo ambao ulifanywa na Polisi kwa kushirikiana na wananchi wa eneo la
Maili kumi ndipo walipobaini kuwepo kwa vifaa vingine katika nyumba mbili
tofauti za ibada zilizopo Kijijini hapo.
Alisema watuhumiwa hao baada ya mwenzao kukamatwa
walikimbia kujificha kwenye nyumba hizo za ibada ndipo wakazi wa maeneo hayo
walipowatilia mashaka na kutoa taarifa kwa Polisi.
“Baada ya kukimbizwa wakaona mahali salama kwao ni
kwenye nyumba za ibada lakini wananchi wa eneo lile waliwatilia shaka na kuamua
kutoa taarifa ndipo yalipokutwa hayo mabomu ambayo yalikuwa yameshaandaliwa
kulipuka kwani kulikuwa na petrol na tambi ndani ya chupa hizo na zile gololi
hutumika kama silaha zinapolipuka”,alifafanua Kamanda Massawe.
Hata hivyo kwa mujibu wa Kamanda huyo ni kwamba
baada ya mahojiano ya Polisi na watuhumiwa hao walibaini kuwa ni miongoni mwa
wale waliokimbi katika oparesheni ya kuwasaka wahalifu iliyofanyika mwishoni
mwa mwezi Novemba mwaka huu huko wilayani Kilindi.
“Hawa ni miongoni mwa wale waliosababisha machafuko
wilayani Kilindi ambapo Mgambo aliuawa sasa wengine walikimbia na inaonekana
nao hawa wapo katika mtandao huo”,alisema.
Kamanda Massawe alitoa wito kwa wakazi wa
mkoa wa Tanga kutoa taarifa mara moja kwa Polisi mara wanapobaini kuwepo kwa
watu ambao wanawatilia mashaka kwenye maeneo yao.
No comments:
Post a Comment