![]() |
| Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas akiwaonyesha waandishi wa habari (Hawapo pichani) noti bandia zenye thamani ya Tsh 6,140,000 ambazo zilikamatwa maeneo ya Kituo kikuu cha Mabasi cha jijini hapa ambapo mtuhumiwa alikuwa anataka kuzisafirisha kwenda Dar es salaam. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha) |
Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani hapa limemkamata mwanamke mmoja aitwaye Imelda
Juma (20) Mkazi wa Sokoni One jiji hapa akiwa na noti bandia zenye thamani ya
Tsh 6,140,000 (Milioni sita laki moja na elfu orobaini).
Akiongea na waandishi
wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba tukio hilo lilitokea
tarehe 13.12.2013 muda wa saa 10:00 Alasiri katika maeneo ya Kituo kikuu cha
Mabasi mara baada ya jeshi hilo kupata taarifa toka kwa raia wema.
Kamanda Sabas
alifafanua kwa kusema kwamba, siku ya tukio mtuhumiwa ambaye ni Imelda Juma
alimtuma dereva wa pikipiki maarufu kama “boda boda” aitwaye Jamal Abdul ili
aende maeneo ya Sakina Darajani kwenda kuchukua mzigo. Mara baada ya dereva
huyo kufika katika eneo hilo aliukuta mzigo huo ukiwa pembeni ya pikipiki
nyingine ambayo haikuwa na mtu.
Dereva huyo wa
pikipiki aliuchukua mzigo huo na kuupeleka katika kituo cha mabasi cha Dar
Express kama alivyoelekezwa na mtuhumiwa ambaye ndio mmiliki wa mzigo huo ili
autume kwa mtu aliyefahamika kwa jina moja la Emmanuel ambaye inadaiwa yupo Dar
es salaam.
Wafanyakazi wa
kampuni ya mabasi ya Dar Express waliokuwa ofisini hapo hawakuwa tayari kuupokea
na kuusafirisha mzigo huo bila kuufungua ili wajiridhishe japokuwa dereva wa
boda boda alikataa kufungua mzigo huo kwa madai kwamba mwenye mzigo alimwambia
hasikubali mzigo huo ufunguliwe.
“Ndipo wafanyakakazi
hao wakamshauri dereva huyo wa boda boda kama hataki ufunguliwe basi naye pia
akate tiketi ili asafiri pamoja na mzigo wake mpaka Dar es salaam”. Alisema
Kamanda Sabas.
Mara baada ya taarifa
hiyo kufika katika kituo kikuu cha Polisi, askari waliweka mtego na kumkamata
mtuhumiwa huyo Imelda Juma ambaye inasemekana alikuwa maeneo ya karibu na hapo.
Mpaka hivi sasa Jeshi
hilo linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo ili kuweza kubaini mtambo unaotengeneza
fedha hizo bandia huku pia likiendelea kumtafuta mtumiwa mwingine aitwaye
Emmanuel.
Kufuatia tukio hilo
Kamanda Sabas ameendelea kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu kwa jinsi
wanavyoshirikiana na jeshi hilo juu ya utoaji wa taarifa kwani fedha hizo kama
zingesambaa mtaani kwa ajili ya matumizi zingedhoofisha uchumi wa nchi kwa
kiasi fulani.
Aidha amewatahadhalisha
wananchi wa Mkoa huu hasa wafanyabiashara kuwa makini na noti mbalimbali
wanazozipokea toka kwa wateja wao, kwani wengine hutumia mwanya wa wingi wa
noti kupenyeza fedha bandia.

No comments:
Post a Comment