![]() |
| Dkt Kitila Mkumbo |
Kwa siku za karibuni, vyombo mbalimbali vya habari
hapa nchini vimetoa taarifa kuhusu kuvuliwa uongozi kwa Dkt. Kitila Mkumbo
ndani ya chama cha siasa kiitwacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA).
Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, Dkt. Mkumbo
alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA.
Taarifa hizo zimeushtua uongozi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam kwa sababu zimekuwa tofauti na ilivyokuwa ikieleweka kuhusu
uhusiano uliokuwepo baina ya Dkt Mkumbo na CHADEMA.
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unapenda
kutoa taarifa kwa umma kuwa, kwa mujibu wa Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma
uliotolewa mwaka 2000 ni marufuku kwa mfanyakazi wa umma kuwa kiongozi, au kuwa
na madaraka yanayofanana na uongozi, katika chama chochote cha siasa. Kwa
upande mmoja, Waraka huo uko wazi na wafanyakazi husika wanaufahamu, na wale
wanaoonyesha dalili za kutetereka hukumbushwa au kuonywa; wanaokaidi
huchukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Kwa msingi huo, na kwa kuzingatia kuwa Dkt.
Mkumbo hajawahi kujibainisha rasmi kama kiongozi ndani ya CHADEMA, Chuo
hakikusita kumpitisha kuwa Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu Kishiriki
cha Dar es Salaam kuanzia mwaka 2012. Kabla ya hapo, Dkt. Mkumbo alikuwa Mkuu
wa Idara ya Saikolojia ya Elimu na Taaluma za Mitaala katika Shule Kuu ya
Elimu, Kampasi ya Mwalimu Nyerere – Mlimani (2009-2012).
Kwa upande mwingine, pamoja na wingi wa taarifa hizo
za vyombo vya habari, Dkt. Mkumbo amekanusha kimaandishi tuhuma hizo za kuwa
mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA, na kusisitiza kuwa yeye alijiuzulu nafasi hiyo
ya ujumbe wa kamati kuu tangu Januari 2010, baada ya kutanabaishwa juu ya
sheria husika, na kwamba hajawahi kuurejea wadhifa huo.
Baada ya kupata taarifa za vyombo vya habari
zinazomhusisha Dkt. Mkumbo na nafasi ya uongozi katika CHADEMA, Uongozi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam umelazimika kuchukua hatua ya dharura dhidi ya Dkt.
Mkumbo, kwa kumsimamisha kutoka kwenye nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo Chuoni.
Lengo na manufaa ya hatua hii ni kama ifuatavyo.
Kwanza, kupitia kamati maalum iliyoundwa, Chuo
kitapata fursa ya kufanya uchunguzi yakini utakaobainisha ukweli wa jambo hilo.
Pili, hatua hii itampa Dkt. Mkumbo fursa ya kujitetea katika ngazi zote
zinazohusika, akiwa huru na bila kuathiri utendaji kazi wa ofisi yake. Tatu,
hatua hii itaiwezesha kamati husika, pamoja na Dkt. Mkumbo mwenyewe, kufanya
kazi zao za uchunguzi na utetezi bila kuingiliwa au kuathiriwa na cheo au
madaraka aliyokuwa nayo Dkt. Mkumbo.
Baada ya hatua hiyo, Dkt. Mkumbo amemwomba Makamu
Mkuu wa Chuo kwa maandishi amruhusu ajiuzulu wadhifa wake wa Mkuu wa Kitivo na
ombi hilo limekubaliwa tarehe 3 Desemba 2013.
Pamoja na hayo, inabidi ieleweke kuwa Dkt. Mkumbo
amejiuzulu uongozi, na siyo kazi; yeye bado ni mhadhiri mwandamizi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, izingatiwe kuwa suala la uchunguzi linaendelea,
na kamati hiyo ya uchunguzi imepewa jukumu la kuchunguza na kubaini ukweli, na
kisha kutoa mapendekezo kwa uongozi wa Chuo.
Mara baada ya mapendekezo hayo, na baada ya
Dkt. Mkumbo kupewa nafasi ya kujitetea na kusikilizwa, uongozi wa Chuo utatoa
uamuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unauomba
umma kuwa na subira katika jambo hili. Kadhalika, wale watakaosailiwa na Kamati
iliyoundwa tunawaomba watoe ushirikiano wa dhati ili kubainisha ukweli na
kuharakisha mchakato wa uchunguzi. Tunaamini kuwa penye ukweli, uwongo daima
hujitenga, na hivyo katika hili, ukweli utadhihirika na hatimaye haki
itatendeka.
Imetolewa na
Prof. Yunus D. Mgaya
NAIBU MAKAMU MKUU WA CHUO – UTAWALA NA AFISA
MNADHIMU WA CHUO KIKUU
3 Desemba 2013

No comments:
Post a Comment