| Kamanda Massawe |
Na Mwandishi Wetu Tanga
ZAIDI ya kesi za ubakaji 300 zimeripotiwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe, alisema kati ya kesi hizo 148 bado ziko kwenye upelelezi na 100 zinaendelea mahakamani ambapo 13 zilipata ushindi kwa washtakiwa kupatiwa adhabu ya mahakama.
Alieleza kesi tano zilishindwa mahakamani wakati 42 zilifungwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na ushahidi wa kuweza kupeleka kesi hizo kwa mwanasheria wa serikali kwa hatua za kisheria.
Kamanda Massawe alisema a kwa upande wa makosa ya kulawiti 46 yaliripotiwa katika vituo vya polisi mkoani hapa ambapo alisema kesi 18 ziko katika hatua ya upelelezi wakati 16 zikiwa mahakamani na moja ilipata ushindi mahakamani na mshtakiwa kupatiwa adhabu huku kesi moja ikishindwa mahakamani na 10 zikifungwa kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa upande wa makosa ya kutupa watoto, manne yaliripotiwa ambapo kesi zote nne zilifungwa kutokana na sababu mbalimbali.
Aidha, Kamanda Massawe alisema jeshi la polisi mkoa wa Tanga kupitia Dawati la Jinsia na Watoto linaendelea kupokea kesi zinazojenga makosa ya jinai na zile ambazo zimekuwa na asili za makosa ya madai.
No comments:
Post a Comment