Tanga.
MZEE wa Miaka sabini anashikiliwa na
jeshi la polisi kwa tuhuma za kuoa binti mwenye umri chini ya miaka kumi na
nane Mosa Hamisi kinyume cha sheria zilizopo hapa nchini.
Mkasa huo ulitokea Novemba 10 mwaka huu
majira ya saa kumi na moja jioni ambapo mzee huyo tayari alishafunga ndoa na
binti huyo lengo likiwa ni kuishi naye kama mke na mume.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Tanga,Constatine Massawe amethibitisha kutokea tukio hilo na kueleza tayari
jeshi linamshikilia mtuhumiwa huyo pamoja na mama mzazi wa binti huyo.
Massawe alimtaja mzee huyo kwa jina la
Abdallah Tuppa (70)mkazi wa barabara kumi mbili na mama mzazi binti huyo Batuli
Tupa (35)ambaye anaishi barabara kumi na nne jijini Tanga.
Alisema tukio hilo liligunduliwa na
wasamaria wema baada ya kuona binti huyo anaozeshwa ndipo walipoamua kutoa
taarifa kwa jeshi la polisi ambapo wakati polisi walipofika eneo hilo walimkuta
mzee huyo akidai mke wake ndipo walipomkamata.
Kamanda Massawe alisema askari
walifanikiwa kumuhoji binti huyo ambapo alisema umri wake ni zaidi ya miaka
kumi na saba hali ambayo ilipelekea kumuambia alete cheti chake cha kuzaliwa
ili kuthibiti umri huo.
Wakati huo huo,mtu mmoja amekufa baada
ya kugongwa na gari akiwa anaendesha baiskeli katika barabara ya Segera
–Chalinze.
Kamanda Massawe alisema tukio hilo
lilitokea juzi majira ya saa 3 za usiku na kumtaja dereva aliyesababisha ajali
hiyo kuwa ni Abdallah Msangi (30) wa gari hilo aina ya fuso lenye namba T390
DCB.
Massawe alimtaja aliyefariki katika
ajali hiyo kuwa ni Hamisi Saidi mkazi wa Michungwani ambapo alisema chanzo cha
ajali hiyo ni uzembe wa dereva.

No comments:
Post a Comment