Serikali ya
Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Kampuni ya Total wamekubaliana
kuharakisha hatua zote za awali katika Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda
hadi Hoima Tanga ili shughuli za ujenzi rasmi zianze mwezi Mei mwaka huu.
Makubaliano hayo yalifikiwa Alhamisi, Februari 1, wakati Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani alipokutana na uongozi wa juu wa kampuni hiyo
wizarani Dodoma.
Aidha, makubaliano mengine yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kuwa kazi
za awali za maandalizi ya ujenzi ziwe zimekamilika ifikapo mwezi Machi mwaka
huu.
“Ni lazima tuharakishe mchakato huu kama Mheshimiwa Rais Magufuli
alivyoagiza. Hivyo, tumekubaliana kwamba shughuli zote za maandalizi ziwe
zimekamilika ifikapo Machi mwaka huu ili kuwezesha shughuli rasmi za ujenzi wa
Bomba kuanza mwezi Mei,” alifafanua Waziri Kalemani.
Vilevile, katika kikao hicho, Rais wa Kampuni ya Total sehemu ya
Afrika, Guy Maurice ambaye alikuwa kiongozi wa Ujumbe huo, alibainisha nia ya
kampuni yake kuwekeza katika shughuli nyingine mbalimbali zinazohusiana na
Mradi wa Bomba jambo ambalo alisema litainufaisha zaidi Tanzania.
Mbali na makubaliano yote yaliyofikiwa, Waziri Kalemani pia alisisitiza
kuwa ni muhimu kampuni ya Total iwasilishe Mpango-Kazi wake wizarani mapema
iwezekanavyo ili utumike kama mwongozo-rejea katika kutathmini utekelezaji wa
Mradi huo mkubwa.
Kampuni ya Total ndiyo mwekezaji katika utekelezaji wa Mradi wa ujenzi
wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Hoima, Tanga.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt.
Hamisi Mwinyimvua, Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara Lusius Mwenda,
Mkurugenzi wa Sera na Mipango Haji Janabi na maafisa wengine waandamizi kutoka
wizarani.
No comments:
Post a Comment