MAMLAKA
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepiga marufuku uingizaji na usambazaji wa simu
za mkononi za Smartphone Samsung Galaxy note 7 kwa kuwa zina matatizo ya betri.
TCRA pia imewataka wananchi ambao
tayari wanatumia simu hizo kuzizima na kuzirudisha haraka katika maduka
walikozinunua.
Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent
Mungy, amewataka watanzania wajihadhari kuitumia simu hiyo kwa kuwa Kampuni ya
Samsung yenyewe imeiondoa sokoni.
“Simu hiyo tayari Samsung wenyewe
wamesema ina matatizo ya betri na mara mbili sasa imelipuka,” amesema Mungy.
Amewaomba watu wenye simu za aina
hiyo kuzirudisha madukani haraka wabadilishiwe ama kurudishiwa fedha zao.
“Hata kama uliletewa zawadi kutoka
nje ya nchi nawaomba warudishe huko kuepuka matatizo yanayoweza
kujitokeza,” amesema Mungy.
Hivi karibuni simu aina hiyo
iliyothibitishwa na kampuni hiyo kuwa ilikuwa salama, ilishika moto kwenye
ndege nchini Marekani.
Simu hiyo inadaiwa kushika moto
ikiwa mikononi mwa abiria aliyekuwa kwenye shirika la ndege la Southwest
Airlines.
Shirika hilo liliwaondoa kwa dharura
abiria waliokuwa kwenye ndege iliyokuwa imepangiwa kusafiri kutoka
Louisville, Kentucky, hadi Baltimore, Maryland muda mfupi kabla ya kupaa.

No comments:
Post a Comment