Mbunge wa
Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), kushoto akizungumza na Waziri Mkuu Mh Mizengo Pinda.Picha na Maktaba
|
Hata hivyo ombi hilo litapatiwa majibu na kiti cha Spika, baada ya Kamati ya Uongozi ya Bunge kukutana jioni jana kujadili masuala mbalimbali ambapo Naibu Spika, Job Ndugai alisema suala hilo ni miongoni mwa mambo yaliyotarajiwa kujadiliwa na kutolea uamuzi.
Awali katika mwongozo wake, Mpina aliomba Mkutano huo wa 16 na ule wa 17 inayofanyika kwa pamoja kuanzia jana hadi Novemba 28, mwaka huu, kuahirishwa ili fedha walizopaswa kulipwa wabunge zitumike kununua dawa.
Mwongozo wa Mpina ulikuja baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Al – Shaymaa Kwegyir (CCM) kutaka kujua sababu za kuchelewa kupatikana kwa dawa katika vituo vya afya nchini na pia MSD kuidai Serikali kiasi kikubwa cha fedha bila kulipwa kwa muda mrefu sasa.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na swali la Mheshimiwa Al-Shaymaa, kuhusu mabilioni ya fedha ambayo MSD inaidai Serikali na kusababisha uhaba mkubwa wa dawa katika hospitali nyingi nchini, sisi kama Bunge hatuwezi kukaa kimya.
“Kimsingi hali katika hospitali zetu ni mbaya sana, ukienda pale Muhimbili (Hospitali ya Taifa) hakuna dawa kabisa. Lakini pia ukienda katika hospitali kubwa zote hakuna dawa. Watoto wetu, mama zetu na wazee wetu wanakufa ovyo hivi sasa kutokana na ukosefu wa dawa.
“Mwongozo ninaouomba kwako Mheshimiwa Naibu Spika ni kwa Bunge kuahirisha mkutano huu wa 16 na wa 17 ili fedha hizi sasa ziende zikanunue dawa na kuwaokoa wananchi wetu,” alisema Mpina.
Akijibu hoja hiyo iliyoonekana kuungwa mkono na wabunge wengi, Ndugai alisema suala hilo lingejadiliwa katika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge iliyotarajiwa kukutana jana jioni.
“Kwa hiyo waheshimiwa wabunge baada ya kikao hiki kulijadili suala hilo kwa upana wake, tutakuja kuwaeleza nini maoni au ushauri wa kamati kwa suala hilo,” alisema Ndugai.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment