| MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA JIJI LA TANGA,JULIANA MALANGE KULIA NA KUSHOTO NI NAIBU MSTAHIKI MEYA WA JIJI LA TANGA,SHEMDOE |
UKOSEFU wa gari la wagonjwa katika
kituo cha afya Pongwe kilichopo kwenye Halmashauri ya Jiji la Tanga
unasababisha mazingira magumu ya kuwasafirisha wagonjwa wanaohitaji huduma
zaidi za kimatibabu kutoka maeneo ya mbali na kituo hicho.
Akizungumza katika hafla fupi ya
wafanyakazi kujipongeza kwa mafanikio waliyopata kwa utoaji wa huduma
bora zikiwemo za wajawazito na watoto, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk.
Faisal Ali, alisema wamepokea wagonjwa kutoka vijiji mbalimbali na baadhi yao
kuwa na kesi za kupata tiba hospitali nyingine, hivyo huwa vigumu
kuwasafirisha.
“Hiki kituo unaweza kukiona ni
kidogo ila kiutendaji ni kikubwa, hakuna mtu ambaye hajui kama tunahudumia
mamia ya watu kwa siku, tatizo ni pale mgonjwa au mjamzito tunapotaka kumpeleka
Hospitali ya Bombo ndiyo balaa, hatuna gari,” alisema Dk. Ali.
Aliiomba serikali kupeleka gari la
wagonjwa katika kituo hicho ili kukabiliana na changamoto za wajawazito wakati
wa kujifungua na utoaji wa elimu ya umuhimu wa kuhudhuria kiliniki.
Kwa mujibu wa Dk. Ali, baadhi ya
wanawake hasa wa vijijini hawajui umuhimu wa kuhudhuria kliniki ili kujua
mwenendo wa ujauzito.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Katibu Msaidizi Afya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Yombo Shelufumo,
aliwataka wafanyakazi hao kutobweteka na mafaniko waliyoyapata na kuwaasa
kufanya kazi kwa bidii ili kuyafikia mafanikio zaidi.
Alisema mbali ya changamoto nyingi
wanazokabiliana nazo, zikiwemo za kupandishwa vyeo na umbali wa wafanyakazi
wanapoishi, serikali inatambua na hivyo kuwataka kufanya kazi kwa bidii.
Shelufumo alisema siri ya mafaniko
ni kufanya kazi kwa bidii, na hivyo kuwataka kufanya uvumilivu huku serikali
ikitambua changamoto hizo na kuzifanyia kazi zikiwemo za kuwapandisha vyeo.
No comments:
Post a Comment