![]() |
|
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Seif Rashidi akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, kuhusu maadhimisho ya wiki
ya afya ya Figo itakayoanza tarehe 10 hadi 14, na kuadhimishwa
kitaifa tarehe 13 mjini Dodoma katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, kauli
mbiu ya maadhimisho hayo ni “Figo huzeeka , kadiri mtu anavyozeeka.
Jali afya ya Figo zako”.( Lorietha Laurence-Maelezo)
|
Na Lorietha Laurence-Maelezo
Asilimia 1.03 ya vifo hutokana na ugonjwa wa figo, hayo yalisemwa
na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Seif Rashidi alipokuwa akitoa
tamko kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam,kuhusu siku
ya afya ya figo itakayoadhimishwa tarehe 13 Machi,mwaka huu mjini
Dodoma.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo “Figo huzeeka, kadiri mtu
anavyozeeka. Jali Afya ya Figo zako”. Lengo ni kuelimisha jamii
ili iweze kuelewa umuhimu wa figo katika mwili,
watu kubadili staili za maisha, kuhamasisha watoa huduma kuhusu
wajibu wao katika kugundua magonjwa ya figo na kupunguza hali hatarishi za
ugonjwa sugu wa figo na kuandaa mikakati madhubuti ya kukinga na kuthibiti magonjwa
ya figo.
“ Nawasihi watu wawe na taratibu za kufanya vipimo mara kwa mara,
pia kujali afya zao kwa kuwekeza katika maendeleo ya afya zao ili kujikinga na
ugonjwa wa figo” alisema Mhe.Rashidi .
Aliongeza kuwa ugonjwa huo husababishwa na shinikizo la
damu,ugonjwa wa kisukari na kutokufanya mazoezi mara kwa mara,msongo wa
mawazo,unywaji pombe, unene uliokidhiri,ulaji usiofaa , matumizi ya
chumvi na mafuta pamoja na uvutaji sigara.
Alifafanua kuwa ugonjwa huo
unaweza kumuathiri mtu yeyote aliye katika umri wowote, ingawa
hujitokeza zaidi kwa watu wenye umri wa miaka 50, ambapo takwimu zinaonyesha
kuwa kati ya mwanaume mmoja kati ya watano na mwanamke mmoja kati ya
wanne wenye umri wa miaka 65 hadi 74 wana ugonjwa wa figo.
Pia alieleza kwamba figo ni kiungo muhimu katika mwili
wa binadamu, husaidia katika kuchuja na kuondoa taka mwilini
,majimaji yaliyozidi na kudhibiti kiwango cha kemikali mwilini kwa
kudhibiti shinikizo la damu.
Aliwataka watu waepukane na ugonjwa huu wa figo, kwa kufuata
ushauri wa wataalama na kuzingatia mazoezi, kunywa glasi
6 hadi 8 za maji kwa siku,kuepuka matumizi ya sigara na bidhaa zinazotokana na
tumbaku, kuzingatia maelekezo ya wataalam, kutumia dawa kwa usahihi na
kufuatilia kiwango cha sukari mwilini.
Maadhimisho ya afya ya figo duniani yalianza mwaka 2006,ambapo
mwaka huu yataadhimishwa kuanzia tarehe 10 hadi 14 Machi, katika viwanja vya
Mwalimu Nyerere mjini Dodoma,shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kutoa huduma
ya kupima afya ya figo,kutoa ushauri nasaha na kutoa tiba na rufaa.

No comments:
Post a Comment