TFF
MPYA:
ANGETILE OSIAH LIKIZO,
WAMBURA
KAIMU KATIBU MKUU!!
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemteua Bw. Boniface Wambura kuwa Kaimu Katibu
Mkuu wa TFF. Uteuzi huo ni kuanzia Novemba 2 mwaka huu.
Aidha aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF,
Angetile Osiah ameagizwa aende likizo ya malipo hadi atakapomaliza mkataba
wake.
Kamati ya Utendaji inaviomba vilabu,
vyama vya wilaya, vyama vya mikoa, vyama shiriki na wadau wote kumpa
ushirikiano Bw. Boniface Wambura katika utekelezaji wa majukumu yake.
Jamal Malinzi
Rais
Dar es Salaam
Novemba 3, 2013
++++++++++++++++++++++++++++++++++
HABARI ZA AWALI:
TENGA AKABIDHI, KILA
KITU HADHARANI, SAFI…!!
>>RAIS WA TFF
MALINZI AHUTUBIA….!!
PATA TAARIFA KAMILI:
TENGA AKABIDHI, KILA KITU HADHARANI, SAFI…!!
TAARIFA YA
MAKABIDHIANO YA OFISI YA TFF YALIYOFANYIKA KATIKA OFISI ZA TFF JIJINI DAR ES
SALAAM TAREHE 2 NOVEMBA 2013
Mheshimiwa Rais wa TFF,
Pongezi na Shukurani
1.
Naomba nianze kwa kushukuru kwa kukubali kufanyika kwa shughuli hii ya
makabidhiano ya Ofisi. Utaratibu huu haupo kikatiba wala katika kanuni zetu,
lakini ni muhimu sana kwa vile unatoa taswira ya uongozi endelevu na
ushirikiano unaostahili kuwepo baina ya uongozi mpya na ule wa zamani.
2.
Aidha napenda, kwa mara nyingine, kukupongeza kwa dhati wewe binafsi kwa
kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Shirikisho letu pamoja na kumpongeza Makamu wa
Rais na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa ushindi wao.
3.
Tumeshuhudia mchakato wa uchaguzi uliofanyika kwa uwazi, na ulio huru na wa
haki. Ninawashuru sana na kuwapongeza Wajumbe wa Kamati ya Uchanguzi kwa ueledi
na kazi nzuri walioifanya. Kwa kiwango hicho hicho ninawapongeza na kuwashukuru
Wajumbe wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wa Kamati za Maadili – ngazi ya
awali na ya rufani – kwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu na vyema.
4.
Nawajibika kutoa pongezi kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kukamilisha kazi
muhimu ya kutuchagulia viongozi wetu kwa utulivu mkubwa.
5.
Utulivu wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi – kuanzia mwanzo hadi mwisho – ni
kielelezo cha ukomavu wa uongozi wa mchezo wa mpira wa miguu nchini. Natoa
shukurani za dhati kwa wanachama na wadau wote wa mpira wa miguu nchini kwa
mchango wao wa hali na mali katika kufanikisha zoezi hili muhimu kwa
mustakabali wa mpira wa miguu nchini.
Dira na Malengo ya
Uongozi Uliopita
6.
Dira ya uongozi uliopita ilikuwa ni kujenga mazingira mazuri na endelevu ya
maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Hii ilitokana na hali ya migogoro
isiyoisha na malumbano ya mara kwa mara yaliyokuwepo kabla ya kuingia
madarakani.
7. Ili
kufanikisha dira yetu, uongozi uliopita ulidhamiria kujenga msingi bora wa
uongozi wa mpira wa miguu nchini, hivyo kujiwekea malengo yafuatayo:
Kutengeneza Katiba mpya na Kanuni
zitakazokidhi mahitaji ya nchi yetu ya kudumisha demokrasia na utawala bora –
uwazi, uwajibikaji, na kadhalika.
Kuhakikisha kuwa Katiba yetu na Kanuni
zetu zinazingatiwa na kuheshimiwa.
Kuweka Kanuni za Fedha na kuchukua
hatua za kujenga uaminifu katika usimamizi wa ukusanyaji, utunzaji na matumizi
ya fedha. Tuliazimia kuona hesabu za Shirikisho zinakaguliwa na wakaguzi wenye
sifa za kimataifa, na taarifa ya ukaguzi kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu kila
mwaka, bila ya kukosa.
Kuwa na mfumo wa mashindano utakaongeza
ushindani na kuchochea uwekezaji. Azma ilikuwa ni kuongeza idadi ya mashindano
ili kutoa fursa kwa vipaji kuonekana na kuendelezwa.
Kuweka jitihada katika mafunzo ya
wataalamu wa mpira wa miguu nchini kwa kuongeza idadi na kozi/semina za mafunzo
ya uongozi, uamuzi, ualimu na udaktari wa michezo.
Kujenga mfumo mpya wa uongozi wa timu
za taifa. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha kuwa timu za taifa zinakuwa na uongozi
wake chini ya Mwalimu/Walimu wa timu ya taifa na kuzitofautisha na Idara ya
Ufundi, pamoja na kuhakikisha timu zetu za taifa zinashiriki michezo mingi
iwezekanavyo ya mashindano na ya kirafiki.
Kujenga uhusiano mzuri na wadau na
washirika wetu, hususan wadau wetu wakuu ambao ni Serikali na vyombo zake;
Mashirikisho ya mpira tuliyojumuika nayo - FIFA, CAF, na CECAFA; Wadhimini na
Wafadhili wetu – kampuni, mashirikia ya umma na watu binafsi - wanaochangia maendeleo
ya mpira wa miguu nchini kwa hali na mali.
Kuwa karibu na jamii na kuisaidia
jamii. Nia ni kutumia umaarufu wa mchezo wa mpira wa miguu nchini kuhamasisha
maendeleo ya jamii, hasa katika masuala ya afya ya jamii – kampeni ya malaria,
ukimwi, kupambana na madawa ya kulevya na kadhalika. Rais anayeondoka
madarakani ni Balozi wa Malaria nchini na Rais wetu mpya ni mjumbe wa Kamati ya
Kitaifa ya Kupambana na Malaria, chini ya Uenyekiti wa Waziri wetu wa Afya,
Mheshimiwa Hussein Mwinyi.
8.
Utekelezaji wa Dira tuliyojiwekea na malengo yetu ulifanyika kwa ushirikiano wa
karibu na wanachama na wadau wetu. Yaliyofanyika yanajulikana. Itoshe kusema
kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa jitihada kubwa na uadilifu mkubwa na kwamba
malengo tuliyojiwekea yalifikiwa.
9.
Katika hotuba niliyoitoa katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu uliopita – Jumamosi,
tarehe 26 Oktoba 2013, niliainisha kwa kina nini kilifanyika katika kipindi cha
uongozi uliopita pamoja na mafanikio ya kazi iliyofanyika. Napenda
kuimbatanisha hotuba hiyo kama sehemu ya taarifa hii ya makabidhiano.
10. Matarajio
yetu ni kuwa, baada ya jitihada za kuweka msingi wa uongozi na wa maendeleo ya
mpira wa miguu nchini, nguvu itaelekezwa katika kukuza kiwango cha mpira wa
miguu nchini mwetu. Tulichokifanya ni kutayarisha Mpango wa Muda Mrefu wa
Maendeleo ya Mpira Miguu Nchini – 2013 hadi 2016 (Long Term Technical
Development Plan – 2013 to 2016), ambayo umeambatanishwa kama sehemu ya
taarifa hii ya makabidhiano.
11. Hivyo basi,
uongozi mpya una kazi ya kusimamia na kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo.
Pia, ni matarajio yetu kuwa uongozi mpya utayadumisha mambo ya msingi
tuliyojiwekea na kuufanyia kazi upungufu uliopo.
Shukurani kwa
Wanachama na Wadau wa TFF
12. Pamoja na kuwa
nimeshatoa shukurani mara kadhaa, napenda kwa mara nyingine tena kuwashukuru
wote waliotusaidia kufika hapa tulipo. Nawashukuru sana wanachama wetu, wadau
wetu wote – Serikali yetu na vyombo vyake vyote, wadhamini na wafadhili, waandishi
na vyombo vya habari, wapenzi wa mpira na wananchi kwa ujumla kwa mchango wao
wa hali na mali. Bila yao tusingefika hapa tulipofika.
13. Shukurani maalum
zimwendee Mheshimiwa Rais wetu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa mchango wake
usiopimika. Alikuwa ni sehemu mabadiliko haya tangu mwanzo, hata kabla ya
uongozi wetu kuingia madarakani. Ametusaidia kwa kiasi kikubwa kuzijenga
timu zetu za taifa siyo tu kwa uamuzi wake wa kulipia mishahara ya walimu wa
timu ya taifa, bali pia kwa kuwahamasisha vijana wetu kwa hali na mali wafanye
vizuri. Sina hakika kuwa yupo Rais mwingine, popote pale duniani, aliye karibu
na mapenzi ya dhati kwa vijana wa timu zake za taifa zaidi ya Rais wetu. Zaidi
ya hayo, Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utawala
bora katika mpira wa miguu nchini na amefanya kila aliloliweza kuona kuwa
kiwango cha mchezo kinapanda na timu zetu zinafanya vizuri. Napenda kutoa
shukurani za dhati kwake kwa uongozi na msaada wake.
Wanachama, Katiba na
Kanuni, Wafanyakazi, Mali na Mikataba ya TFF
14. Wanachama
TFF ina jumla ya Wanachama 44 ambao
wote ni wanachama hai kama ifuatavyo:
Vyama vya Mikoa – 25
Vyama Shiriki
- 5
Vilabu vya Ligi Kuu - 14
15. Katiba
na Kanuni
Hivi sasa TFF ina Katiba Mpya (ya Mwaka
2013) iliyofanyiwa marekebisho ya mwisho na Mkutano Mkuu Maalum wa TFF tarehe
13 Julai 2013.
Pamoja na Katiba TFF ina kanuni
zifuatazo ambazo kwa mujibu wa Katiba ya TFF hupitishwa na kamati ya Utendaji:
Kanuni za Fedha
Kanuni za Mashindano kuanzia Ngazi ya
Wilaya hadi Ligi Kuu
Kanuni za Utii
Kanuni za Nidhamu
Kanuni za Maadili
Kanuni za Uchaguzi za Uchaguzi za TFF
na za Wanachama wa TFF
Kanuni zinazosimamia Uendeshwaji wa
Bodi ya Ligi Kuu
Kanuni za Mashindano mengine, kama vile
Copa Coca Cola, Uhai Cup, Super 8 na Taifa Cup. Ni vyema ikafahamika kuwa kila
mashindano lazima yawe na Kanuni zinazosimamia uendeshwaji wake.
TFF inalazimika kuzifanyia marekebisho
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wake kufuatia marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi
za TFF. Aidha, TFF inadeni la kutayarisha Kanuni za Chombo cha Usuluhishi
(Arbitration Tribunal) kama ilivyoainishwa katika Katiba. Hivi karibuni, TFF
imepokea Kanuni za Mfano kutoka FIFA ambayo ipo haja ya kazi hii kukamilishwa
na uongozi mpya.
16. Wafanyakazi
wa TFF
Hivi sasa TFF ina jumla ya wafanyakazi
29. Kati yao yupo/wapo
Katibu
Mkuu
- 1
Wakurugenzi / Maofisa
Mwandamizi
- 5
Wafanyakazi wengine
- 23
Katibu Mkuu na Wakurugenzi wapo katika
kipindi cha nyongeza cha miezi sita (6) cha mikataba yao, kinachoishia mwishoni
mwa mwezi Desemba 2013. Wafanyakazi wengine wapo katika mikataba ya
miaka minne yenye kipindi cha majaribio cha miezi sita kuanzia mwanzoni mwa
mwezi Septemba 2013. Hivyo basi, uongozi mpya una nafasi ya kufanya tathmini ya
mahitaji ya TFF kisha kufanya uamuzi juu ya ajira za Wafanyakazi waliopo kadiri
utakavyoona inafaa.
TFF ilichukua hatua ya kuingia kufanya
makubaliano ya hiari na wafanyakazi wake ili kuondokana na ajira za maisha
(Permanent Employment) na kubaki na ajira za mikataba (Contract Empoyment) kwa
wafanyakazi wake wote.
Wafanyakazi wa TFF wamekuwa wakifanya
kazi ngumu na saa nyingi kuliko kawaida. Ajira ya TFF haina saa za ziada wala
siku za mapumziko. Kutokana na dhana ya kujitolea na ukweli kwamba shughuli
nyingi za TFF, kama vile michezo na mikutano hufanyika siku za mwisho wa wiki
na sikukuu, ni dhahiri kuwa Wafanyakazi wa TFF wamekuwa wakilazimika kufanya kazi
siku hizo, na mara nyingi bila malipo ya saa za ziada. Aidha, kutokana na
kukosa uwezo, uongozi uliopita ulishindwa kupandisha mishahara yao ipasavyo.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza
na kuwashukuru kwa kuihudumia TFF na mpira wa miguu katika mazingira magumu
sana. Tunauomba uongozi mpya uliangalie suala hili kwa umakini, kama moja ya
hatua za kuongeza ufanisi wa Sekretariati.
17. Mali za
TFF
Hivi sasa TFF ina mali zifuatazo:
Kiwanja cha Karume Stadium, chenye hati
namba 27026 iliyotolewa tarehe 10 Novemba 1981. Kiwanja cha Karume kina ukubwa
wa ekari 8.26. Ombi la kuingezea muda hati hiyo limeshapelekwa na
linafuatiliwa.
Ndani ya Kiwanja hicho, kuna Jengo la
ofisi ya TFF, Jengo la Kituo cha Ufundi (Technical Centre) na Uwanja wa nyasi
za bandia wa Karume.
Kiwanja cha Tanga chenye ukubwa wa
hekta 7.6 (ekari 19) kilichopo katika eneo zuri sana mjini Tanga. Kiwanja hiki
tayari kimeshalipiwa na hivi sasa taratibu zinaendelea kukamilisha taratibu za
kukiandikisha na kupata hati.
Magari sita (6) na Trekta moja (la
kusafishia uwanja wa nyasi bandia). Magari hayo ni: Bus kubwa aina ya Yutong,
basi dogo aina ya Coaster, magari ya aina 4WD Ford Everest, Rav 4, Suzuki
Escudo na Honda CVR. Mawili kati magari hayo - Suzuki Escudo na Honda CVR
– yanatumika lakini hayapo katika hali nzuri. Ni vyema uongozi mpya
ukayafanyia tathmini magari hayo na kufanya maamuzi muafaka kadiri utakavyoona
inafaa.
Fedha taslimu Shilingi 33,518,000 na
US$ 1,390 zipo katika akaunti hivi sasa. Hii ni baada ya TFF kufanya malipo ya
Shilingi 158,000,000 kwa ajili ya Mkutano Mkuu (uliofanyika wiki iliyopita) na
malipo ya Shilingi 56,240,000 yaliyofanyika kwa ajili matayarisho ya Timu ya
Taifa ya Wanawake U-20 na gharama za mchezo baina ya timu yetu ya Taifa na ile
ya Msumbiji uliofanyika wiki iliyopita. Hata hivyo, leo hii US$ 415,000
(Shilingi 664,000,000) kimehamishwa kutoka kwenye Akaunti za TBL kwenda kwenye
Akaunti za TFF. Fedha hizo zitakuwa tayari kwenye Akaunti ya TFF ifikapo
Jumanne wiki ijayo. Malipo haya yalikuwa yafanyike karibu miezi miwili
iliyopita lakini yalicheleweshwa ili kutoa nafasi kwa zoezi la ukaguzi wa fedha
za udhamini wa TBL kufanyika. Zoezi limefanyika vyema na kufikia ukingoni,
ndiyo maana malipo yamefanyika. Malipo mengine yanayofanana na hayo, ya US$ 420,000
(Shilingi 672,000,000) yanatarajiwa kufanyika wiki mbili kutoka sasa - katikati
ya mwezi huu wa Novemba 2013.
Hivyo basi, uongozi unaoingia
madarakani hautaanza kwa shida. Ni matarajio yetu kuwa hatua ya awali itakuwa
kurejesha fedha kwenye akaunti zilikoazimwa kinachofikia US$ 166,509 - US$
148,174 kutoka kwenya Akaunti za FAP na US$ 18,335 kutoka kwenye Akaunti ya TRA
- kwa ajili ya kugharimia Mkutano Mkuu na matumizi ya Taifa Stars kwa ajili ya
matayarisho na safari ya kwenda Gambia.
Ili kujiridhisha kuwa fedha za udhamini
zinatumika kama ilivyokubalika katika mikataba, TFF imetoa nafasi kwa wadhamini
kufanya ukaguzi wa fedha inazozitoa wakati wowote ule. Utamaduni huu tumekuwa
nao katika kipindi chote cha utawala wa uongozi wetu, ili kutoa imani kwa wadhamini
na kuhakikisha kuwa malengo ya udhamini husika yanafanikiwa. Huu ni utaratibu
mzuri na ni matumaini yetu kuwa utadumishwa.
Jengo la Kituo cha Ufundi ndiyo kwa
limekamilika kukarabatiwa na bado halijafunguliwa rasmi. Ukarabati huo
umefanikisha kutengenezwa kwa mfumo wa maji machafu unaojitegemea. Hivyo,
kutohitaji kutengemea mashimo ya Jengo la Ofisi za TFF. Hatuo ya mwisho ya kazi
hiyo ni kukamilisha ukaguzi wa matumizi yaliyofanyika katika ukarabati huo na
kuiwasilisha CAF mapema iwezekanavyo. Hayo ndiyo makubaliana kuhusiana na
msaada uliotolewa na CAF – unaojulikana kama CAF FAP 2.
Ukarabati wa Kituo cha Ufundi
umefanywa, pamoja na sababu nyingine, ili kutoa fursa kwa Mradi wa Ujenzi wa
Karume kuendelea. Kama nilivyoeleza katika Mkutano Mkuu, dhamira ni kuwekeza
katika Mradi wa Ujenzi wa jengo / majengo yenye hadhi kubwa kwa ajili ya
kukodishwa kuzunguka uwanja huo. Jengo lililo karabatiwa na uwanja wa mpira
vitabaki na kuendelea kutumiwa kama Kituo cha Mafunzo. Jambo la muhimu ni
kuhakikisha kuwa uwekezaji katika mradi huo hauhitaji dhamana ya uwanja wetu na
majengo yetu. Ni imani yetu kuwa njia muafaka inapatikana, ikiwa ni pamoja na
utaratibu wa ‘Build, Operate and Transfer’ (BOT).
18. Hesabu
za TFF
Ripoti ya Ukaguzi wa hesabu za TFF hadi
kufikia Desemba 2012 iliwasilishwa katika Mkutano Mkuu uliopita. TFF ilipata
Hati Safi ya Ukaguzi wa hesabu zake na Mkutano Mkuu ukaikubali na kuipitisha
ripoti hiyo hesabu za mwaka 2012. Aidha, taarifa ya hesabu za TFF kwa kipindi
cha kuanzia tarehe 1 Januari hadi 30 Septemba 2013 kusambazwa kwa Wajumbe wa
Mkutano Mkuu.
Ifahamike kuwa TFF imekuwa ikipata Hati
Safi, kila mwaka katika kipindi cha miaka minane iliyopita. Hatuna shaka kuwa
hali hii itaendelea.
19. Mikataba
ya Udhamini
TFF inayo mikataba ifuatayo ya udhamini
na Wadhamini wafuatayo:
Vodacom – Udhamini wa Ligi Kuu
TBL – Taifa Stars
Coca Cola – Mashindano ya Copa Coca
Cola
SSB & Co – Mashindano ya Uhai
Bank ABC – Super 8
Azam Media – Haki za Matangazo ya
Television kwa Ligi Kuu
Aidha, baadhi ya vilabu kama vile Yanga
na Simba vinadhaminiwa na TBL, Coastal Union inafadhiliwa na Tanga Cement
na Azam FC inadhaminiwa na Azam Cola.
Changamoto
zinazoikabili TFF
20. Zipo changamoto
nyingi zinazoikabili TFF lakini kubwa kwa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu
na ambazo uongozi mpya hauna budi kuzishughulikia ni ulazima wa:
Kuendeleza sola la vijana na watoto kwa
kutoa fursa kwa watoto/vijana wengi kupata malezi mazuri ya uchezaji wa mpira
wa miguu ili kupanua wigo wa kupata wachezaji wenye vipaji. Katika jambo hili
bado tuko nyuma sana. Tulididimia sana kutokana na kufutwa kwa michezo
mashuleni. Ipo haja ya uongozi mpya kushirikiana na Serikali kuhamisha michezo
shuleni, kama hatua ya wali ya kutatua tatizo la soka la vijana/watoto.
Kuendeleza soka la wanawake. Matatizo
ya soka la wanawake yanafanana na ya soka la vijana. Tofauti ni ndogo sana.
Kama ilivyo kwa soka la vijana, hatua muhimu kufanyika kwa jitihada ya
kuwahamasisha wasichana wacheze mpira wa miguu shuleni.
Kuhakikisha ueledi unazingatiwa katika
uongozi wa Vilabu na Vyama Wanachama wa TFF. Kinyume chake hatutaweza
kushindana na wenzetu ambao walishapiga hatua katika taaluma ya uongozi wa
michezo. Vilabu vyetu ni lazima vihakikishe kuwa vinatimiza masharti ya
‘Club Licencing’ kama yalivyotolewa na CAF, pamoja na marekebisho yake. Huu ni
mtihani kwetu. Ni lazima tufaulu kutimiza masharti hayo, vinginevyo tutabaki
nyuma. Ipo haja ya kuuangalia kwa mfumo wa uongozi wa Vilabu vyetu na Vyama
Vyetu kwa azma ya kubuni mfumo utakaotuletea ufanisi zaidi wa kiungozi na
uendeshaji kuliko ilivyo hivi sasa.
Kuhamasisha uwekezaji katika maendeleo
ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Tuna upungufu mkubwa wa vifaa na
viwanja vya kuchezea. Ni vigumu kuundeleza mchezo wa mpira bila ya kuwa na
viwanja vya kuchezea na vifaa. Aidha, zinahitajika raslimali watu na fedha
katika kulea na kuwaendeleza wachezaji na wataalamu wetu. Licha ya hapo kiasi
kikubwa cha fedha kinahitajika kwa ajili ya matumizi mengine ili timu ifanye
vizuri. Kwa maneno mengine tunahitaji kufanya kila jitihada kuhamasisha watu
binafsi, makampuni na Serikali iwekeze katika mpira, wadhamini zaidi wajitokeze
na wapenzi wengi zaidi wachangie timu zao – kwa njia mbalimbali - ili kuongeza
mapato ya vilabu na vyama husika. Vilabu vyetu na Vyama Wanachama wa TFF
vinakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha za uendeshaji. Mawazo au fikra
kuwa kuna fedha nyingi katika mpira wa miguu ni dhana isiyo na msingi na
inayotokana na kutofahamu gharama za uendeshaji wa vilabu na vyama vyetu. Pamoja
na ongezeko kubwa la mapato ya milangoni na mchango wa udhamini katika kipindi
cha uongozi uliopita, bado kinachopatikana hakikidhi hata theluthi moja ya
mahitaji muhimu. Haja ya kuongeza mapato ndiyo changamoto mama. Ikitatuliwa
itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makali ya changamoto nyingine.
Ili kuvutia uwekezaji, udhamini na
misaada kwenye mpira wa miguu, ni lazima tuhakikishe kuwa tunaendelea na
jitihada za kujenga uaminifu wa utunzaji na matumizi ya fedha ndani ya TFF. Ipo
haja ya kuhakikisha kuwa Kanuni za Fedha zinazingatiwa na hesabu zetu
zinakaguliwa mara kwa mara. Mpango wa Tiketi za Elektroniki ni muhimu usimamiwe
kwa nguvu zote kwa vile sio tu utatuongezea mapato bali pia utatoa picha ya
uaminifu na ueledi.
Uhusiano na ZFA
21. TFF haina
budi kufanya kila linalowezekana kudumisha uhusino mzuri baina yake na ZFA. TFF
inatambulika na FIFA kama msimamizi wa mchezo wa mpira wa miguu nchini
Tanzania. Lakini ukweli ni kuwa mchezo wa mpira katika visiwa vya Unguja na
Pemba unasimamiwa na ZFA. Hakuna matarajio ya hali hiyo kubadilika. Kwa sababu
hiyo, upo ulazima wa kudumisha uhusiano uliopo na kuhakikisha kuwa ZFA inapata
haki ya kupewa baadhi ya miradi inayotokana na fedha za FIFA – FAP. Kwa vile
fedha hizo hatolewa kwa njia ya miradi, utaratibu tuliokubaliana ni kuhakikisha
kuwa kila mwaka baadhi ya miradi / semina zinafanyika visiwani.
Wakaguzi wa Hesabu za
TFF
22. Hesabu za
TFF zinakaguliwa makampuni ya Ukaguzi wa Hesabu yafuatayo:
TAC Associates – kwa hesabu zote za TFF
KPMG – kwa fedha za FIFA
Bodi ya Wadhamini
23. Mkutano Mkuu wa
Mwaka 2011 uliridhia kuundwa kwa Bodi ya Wadhamini wa TFF na Mkutano Mkuu
uliopita ulipitisha majina ya Wajumbe wa Bodi ya Udhamini kama ifuatavyo:
Said El Maamry
– Mwenyekiti
Mh. Joel Bendera
–
Makamu Mwenyekiti
Dr. Ramadhani Dau
– Mjumbe
Steven Mashishanga
– Mjumbe
Mohamed Abdulaziz
- Mjumbe
Mheshimiwa Rais, napenda kukubidhi
taarifa hii ya makabidhiano leo hii tarehe 2 Novemba 2013 kwa ufahamu na
kumbukumbu za TFF. Tafadhali jisikie huru kuomba ufafanuzi wa jambo lolote
lililomo katika taarifa hii au kuomba taarifa juu ya jambo ambalo kwa bahati
mbaya limesahauliwa. Sekretariati ya TFF inawajibika kutoa ufafanuzi
unaohitajika.
Tunakutakia wewe mwenyewe na uongozi
wako kila la heri na mafanikio katika kuingoza wa TFF kuelekea kule
kunakotarajiwa na wapenzi wa mpira wa miguu nchini. Wadau na wapenzi wote wa
mpira wa miguu wanaoitakia heri nchi yetu wapo nyuma yako.
Leodegar
Tenga
Angetile Osiah
RAIS WA
TFF
KATIBU MKUU WA TFF
TANZANIA FOOTBALL
FEDERATION
HOTUBA YA RAIS WA TFF
KWENYE HAFLA YA MAKABIDHIANO
TAREHE 02 NOVEMBA
2013
Ndugu mgeni rasmi
……..…………………………………………….
Ndugu………………………………….
Mwakilishi wa Wizara
Ndugu………………………………….
Mwakilishi wa BMT
Ndugu………………………………….
Mwakilishi wa wadhamini
Ndugu Leodegar Tenga
Rais aliyemaliza muda wake
Ndugu Said El
Maamry Mwenyekiti mstaafu wa iliyokuwa FAT
Ndugu Muhidin
Ndolanga
Mwenyekiti mstaafu wa iliyokuwa FAT
Wajumbe wa Baraza la Wadhamini
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji
Wafanyakazi wa TFF
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu
mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa hapa leo.
Awali ya yote naomba nichukue fursa hii
kukupongeza Rais wetu uliyemaliza muda wako Ndugu Leodegar Tenga na
Kamati yako ya utendaji . Mliyoufanyia mpira wa Tanzania ni makubwa, historia
haitawasahau. Mmetujengea taasisi imara isiyotetereka, taasisi inayoheshimika
ndani na nje ya mipaka ya nchi hii, nawashukuru na kuwapongeza sana.
Uchaguzi umekwisha. Mchakato ulikuwa
mrefu. Wapo walioshinda na wapo ambao kura zao hazikutosha. Wote tuna kazi moja
tu kujenga mpira. Kama tulikwaruzana kwenye kampeni tusameheane, tuwe kitu
kimoja, tuinyanyue soka yetu. Makundi hayajengi yanabomoa, tuachane nayo.
Ndugu zangu, uongozi wetu ulioingia
madarakani alfajiri ya tarehe 28-11-2013 unakabiliwa na changamoto nyingi.
Nitaelezea changamoto chache zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
Mashindano yanayotukabili.
Tunakabiliwa na mashindano mbalimbali
ya kimataifa. Mfano ni mechi ya marudiano ya U/20 wanawake dhidi ya Msumbiji
wiki ijayo, Mitoano ya mashindano ya Afrika wanawake mapema mwakani, Mashindano
ya Chalenji Novemba mwaka huu, na mashindano ya kufuzu AFCON 2015. Yote haya
yanahitaji maandalizi ya haraka.
Programu ya vijana.
Ilani yangu ya uchaguzi ilielezea azma
ya Tanzania kuomba uenyeji wa fainali za vijana za Afrika U/17 mwaka 2019.
Jambo hili tutalizungumzia kwenye kikao chetu cha utendaji leo. Ili tuwe na
timu nzuri ya kucheza fainali hizo tukiwa wenyeji hatuna budi mwaka kesho
kuunda timu ya Taifa ya U/12 itakayokua pamoja kuelekea 2019. Programu yetu ya
vijana tutakayoiandaa sharti ijielekeze kwenye ratiba hii.
Udhamini wa timu za vijana na za
wanawake
Hii ni changamoto kubwa sana kwa TFF.
Timu zetu za Taifa kuanzia zile za wakubwa hadi za vijana ni brands, na kama ni
brands inabidi ziingizwe sokoni, ziuzwe kwa tunaodhamiria wawe wadhamini wa
hizo timu. Kitengo cha masoko lazima kiimarishwe ili kukabiliana na changamoto
hizi. Mdhamini ni mfanyabiashara, anapotoa pesa kudhamini brand fulani
anategemea matokeo mazuri kwake kwa njia ya kukuza biashara zake. Twende kwa
wadhamini tuwashawishi waone watafaidikia nini (leverage) kwa kudhamini timu
zetu. Tusisubiri waje tuwafuate sisi.
Uwekezaji
Jitihada za haraka lazima zifanyike
kuiongezea TFF uwezo wa kiuchumi. Ni muhimu mtaalam mshauri (consultant)
atafutwe atufanyie mchanganuo wa uwekezaji katika ardhi yetu hii ya Karume ili
tuwekeze kitega uchumi kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano mkuu. Aidha bidhaa
zenye nembo yetu zianze kuuzwa kwa utaratibu maalum ili shirikisho lipate haki
yake.
Kabla sijamaliza kuzungumza, niongelee
suala la fujo viwanjani. Mpira ni dakika tisini. Katika kipindi hicho uamuzi wa
mwamuzi unakuwa ni wa mwisho. Tusifiche upungufu wa timu zetu kwa kujificha
nyuma ya kivuli cha mwamuzi. Waamuzi wakionekana wamefanya makosa yawe ya
makusudi au ya bahati mbaya vyombo vya kuwahukumu vipo, mahakama ya waamuzi sio
mashabiki. Kitendo cha mashabiki kufanya fujo kabla, wakati na baada ya mechi
ya mpira kamwe hakikubaliki mahali popote duniani. Kanuni za FIFA, CAF na
TFF ziko wazi na adhabu zinajulikana. Moja ya adhabu hizi ni timu husika
kucheza kwenye uwanja mtupu usio na mashabiki kama ilivyowatokea Al Ahly na
Zamalek huko Misri au kucheza nje ya uwanja wako kama ilivyowatokea Senegal
ambao baada ya vurugu Dakar, Senegal waliamriwa na FIFA mechi zao za nyumbani
wachezee nje ya nchi na wakachagua kuchezea Morocco.
Ndugu zangu yaliyotokea majuzi Mbeya na
Dar es salaam wote tumeyasikia na wengine miongoni mwetu hapa ni mashuhuda.
Ninasema iwe mara ya kwanza na y a mwisho. Kwenye masuala ya kutekeleza
mahitaji ya kanuni uongozi wangu hautaionea haya klabu yoyote, iwe mpya au
kongwe kwenye ligi yetu. Ni jukumu la viongozi wa klabu kudhibiti wanachama na
wapenzi wao. Tabia ya benchi la ufundi kutoa matamshi yanayoweza kuamsha hisia
za mashabiki ni kinyume na taratibu na kanuni ziko wazi kuhusu jambo hili.
Viongozi wa klabu na mabenchi yao ya ufundi wakishindwa kutekeleza wajibu wao
tusilaumiane.
Ndugu zangu ya kufanya ni mengi katika
kuiendeleza soka yetu. Tunashukuru Mungu kuwa uwezo wa kukabiliana na
changamoto hizi tunao na tuna ari na nia ya kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo ya mpira. Ombi langu kwenu nyote ninaomba ushirikiano wa wadau wote
kuanzia Serikali, Halmashauri, mashirika ya umma na binafsi na NGO’s, nina
imani tukishikamana tutaifikia ndoto yetu ya kuing’arisha Tanzania kimpira
kwenye anga za dunia.
Ahsanteni nawashukuru sana.

No comments:
Post a Comment