![]() |
| Gervas Kadaga |
|
MWANAMKE
mmoja mkazi wa kijiji cha Mahango kata ya Madibila wilayani Mbarali mkoani
Mbeya aliyefahamika kwa jina la Jitihada Mamga(20) ameuawa kwa kuchomwa
kisu na mumewe aliyefahamika kwa jina Gervas Kadaga(25) ambaye pia ni mkazi
wa kijijini hapo.
Tukio hilo
limetokea Novemba 21 majira ya saa
1:00 jioni baada ya kutokea ugomvi baina ya wapenzi hao ambapo marehemu
alikutwa na majeraha tisa ya kisu katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda wa Polisi
mkoa wa Mbeya Bw. Diwani Athumani alisema kuwa marehemu alifia nyumbani kwake
ambapo mtuhumiwa ambaye amelazwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya naye
amejeruhiwa kwa kuchomwa na kisu tumboni.
Hata hivyo Kamanda
Athumani alisema kuwa hadi sasa hakijafahamika chanzo halisi cha ugomvi huo
ambapo Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku
mtuhumiwa akiwa amewekwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali ya rufaa
ya Mbeya alikolazwa.
Akizungumza katika
hospitali ya rufaa alikolazwa mama mkubwa wa Gervas aliyejitambulisha kwa
jina la Martha Lugenge alisema kuwa vijana hawa walikutana Madibila kila
mmoja akiwa katika shughuli zake ndipo walipoamua kuishi pamoja.
Alisema yeye
alipewa taarifa za tukio hilo siku inayofuata na kwamba alipofika alikuta
ndugu wa marehemu wameuchukua mwili wa mtoto wao kwa ajili ya taratibu za
mazishi na kwamba hajui chanzo cha ugomvi uliosababisha wapigane visu.
Mama huyo alisema
kuwa vijana hao hawajawahi kupata mtoto na kwamba hawajaanza kuishi pamoja
muda mrefu; ''Wote ni watoto, kwani wameanza kuishi muda mrefu?
wamekutana kila mmoja akiwa katika kazi zake, ndipo walipoanza kuishi kama
mke na mume,''alisema
Na Mbeya yetu blog
|

No comments:
Post a Comment