Mjamzito mmoja aliyetambulika kwa jina la
Magreth Charles (22), mkazi wa Kata ya Lyabukande Wilaya ya Shinyanga
amejifungulia kwenye korido la Kituo cha Afya cha Lyabukande baada ya kukosa
huduma kutoka kwa wauguzi.
Mjamzito
huyo alilazimika kujifungulia kwenye korido kutokana na wauguzi katika kituo
hicho kugoma kutoa msaada wakidai wako kwenye mapumziko na kumtaka aende sehemu
nyingine.
Mama
mkwe wa mjamzito huyo, Rachel Mpanda alisema walifika kituoni hapo wakitokea
kijiji cha Kizungu jirani na kituo hicho na walielezwa na mtu waliyemkuta kuwa
wauguzi wako mapumzikoni, hivyo hakutakuwa na huduma yeyote.
“Baada
ya muda kidogo tukiwa tunatafuta namna ya kwenda kituo kingine, mwari wangu
alianza kusukuma mtoto, hivyo nikaamua kuomba msaada kwa wapitanjia ili
wamsaidie ajifungue, alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume,” alisema Mpanda.
Diwani
wa kata hiyo, Joseph Misiri alisema tukio la mwanamke huyo kujifungua kwenye
korido si la kwanza na kwamba kuna mwanamke mwingine alikosa huduma hiyo na
kusababisha mtoto kufariki dunia.
“Serikali
haina budi kuwachukulia hatua wauguzi katika kituo hiki kwani wanasababisha
kupoteza maisha ya watoto wachanga, mwishowe watasababisha kupoteza maisha kwa
wajawazito kwa kukosa huduma ya matibabu,” alisema Misiri.
Mmoja
wa wauguzi katika kituo hicho, Zulfa Mussa alisema kituo hicho kina watumishi
watatu; muuguzi mmoja alikuwa amempeleka mgonjwa hospitali ya rufaa, daktari
mfawidhi wa kituo, Kadela Mashaka alikuwa semina na yeye alikuwa zamu usiku,
hivyo alitakiwa kupumika mchana huo.
“Kwa
kawaida aliyekuwa zamu ya usiku anatakiwa kwenda kupumzika kujiandaa na zamu
yake nyingine, hivyo niliondoka kituoni na kumwacha mtaalamu wa maabara,” alisema Zulfa.
Mkurugenzi
wa Halmashauri hiyo, Kiomoni Kibamba alipohojiwa alisema hana taarifa na
kuahidi kufuatilia.
No comments:
Post a Comment