MAUAJI ya Watanzania kwa njia ya
kuchinjwa yanaendelea kushika kasi baada ya usiku wa kuamkia jana wakazi 8 wa
kitongoji cha Kibatini, kata ya Mzizima jijini Tanga kuuawa kwa kuchinjwa
shingo na watu wasiojulikana.
Watu hao ambao inadaiwa
kuwa ni majambazi walivamia usiku wa kuamkia jana kwa kuvunja milango ya nyumba
tatu ambazo wakazi hao walikuwa wamelala na kuwachinja kisha kuiba biskuti,
mchele na sukari na kutokomea navyo kusikojulikana.
Wauaji hao
inadaiwa wana uhusiano na wahalifu ambao wamekuwa wakijificha ndani ya mapango
ya Majimoto na kujihusisha na matukio kadhaa cha uvamizi ili kupora vyakula na
kusababisha mauaji ya wakazi wa Jiji la Tanga, ikiwamo katika duka kuu la
Central Bakery mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Mmoja wa shuhuda
wa mauaji hayo, Kea Leonard (70) ambaye pia ni mkazi wa Kibatini, katika
mahojiano jana alisema wanaamini kwamba chanzo cha mauaji ya wenzao ni kulipiza
kisasi.

Aliongeza kwamba
wakati wahalifu hao wanavamia nyumba ya mjumbe wa serikali ya kitongoji kabla
ya kumtoa nje walisikia mmoja wa watu hao akimhoji kuhusu mahali walipopelekwa
watoto saba.
Diwani wa Kata
ya Mzizima, Fredrick Charles akizungumza na waandishi wa habari na kuthibitisha
kwamba kati ya watu waliokufa mmoja ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mleni
uliopo kwenye kata hiyo.
“Hali ya usalama
hapa kwetu Mzizima si shwari kwa sababu wananchi wangu wa Kibatini wamevamiwa
na kuchinjwa usiku wa kuamkia jana majira ya saa sita usiku,” alisema Chiluba.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mleni kilichopo kitongoji hicho, Shabani
Amani alisema wamepatwa na hofu kubwa kuhusu matukio hayo.
“Tunadhani kuna
mapungufu katika suala la ulinzi hapa kwa sababu baada ya kutokea matukio
kadhaa eneo letu hasa baada ya kudaiwa kwamba mapango waliyojificha wahalifu
yako hapa jirani na kwetu kikosikazi cha mchanganyiko wa askari polisi na wa
JWTZ wanafanya doria kwa saa 24 lakini tunashangaa kwa nini matukio
yanaendelea,” alisema Amani.

Aliwataja waliouawa ni Issa Hussein (50) ambaye ni
mmiliki wa kaya hiyo pamoja na kuibwa biskuti, mchele na sukari katika duka
dogo. Wa kaya nyingine ni Mkola Hussein (40) na Hamis Issa (20), Hamis Issa
(20) na aliyemtaja kwa jina la Mikidadi (70).
Kamanda aliwataja marehemu wengine ni Mahamud (35)
ambaye ni mkwe wa Mikidadi, Issa Ramadhani (25), Kadir (25) na Salum ambao ni
wachunga ng’ombe kijijini humo.
Hata hivyo,
mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mke wa marehemu Mkola aitwaye Aisha Saidi,
alisema walipofika nyumbani hapo waligonga mlango na kumtoa nje Mkola na
kuondoka naye.
Katika hatua
nyingine, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa
kupokea taarifa za vitendo vya mauaji ya kikatili vinavyoendelea kutokea katika
maeneo mbalimbali nchini.
“Wimbi hili la
matukio ya vitendo vya mauaji na ukatili uliojitokeza kwa kufuatana mwezi Mei
2016 yanavunja haki ya kuishi ambayo ndio msingi wa haki zote za binadamu kwa
ujumla wake.
Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali mauaji haya yote na matendo yote ya
kikatili dhidi ya mwanadamu yanapotokea popote nchini,” ilieleza taarifa ya
Mwenyekiti wa Tume, Bahame Nyanduga.
Tume iliishauri
serikali kupitia Jeshi la Polisi ichukue hatua mahsusi kuhakikisha ulinzi wa
wananchi dhidi ya mauaji na vitendo hivi, kwani jukumu la kwanza la kuhakikisha
usalama wa wananchi ni jukumu la serikali. Jeshi la Polisi lihakikishe watu
wote waliohusika kutekeleza mauaji haya wanakamatwa ili sheria ichukue mkondo
wake, ilieleza.
Wakizungumza
katika eneo la tukio baadhi ya waathirika ambao ndugu jamaa na zao wamechinjwa
majira ya saa saba usiku wamesema kundi la watuhumiwa wanaokadiriwa kuwa walikuwa watu nane na kuvalia nguo
nyeusi walipofika katika nyumba zao waliwaamuru akina baba watoke nje kisha
kuwapeleka hadi katika vichaka kisha kuwachinja.
Tukio hilo
limekuja wiki mbili tu baada ya vikundi hivyo vya uhalifu vinavyodaiwa
kujificha katika mapango ya Amboni Mleni Maji moto kuchinja mbuzi 48,ng'ombe
wawili na kuku zaidi ya 12 lakini Kamanda wa Polisi amekiri kuwa tukio hilo ni
kubwa na kwamba jitihada za polisi zinafanywa ili kuhakikisha kuwa watuhumiwa
wanakamatwa na kutiwa mbaroni.
MASWALI
MATANO (5) TATA KUHUSU MKASA HUU
1. Majambazi wanaporaje biskuti na mchele…?
2. Kama shida ni mali waliouwawa walikuwa na hatia gani..?
3. Kwanini matukio haya hayakomi licha ya juhudi zinazotajwa
na vyombo vya usalama kuwa zinaendelea..?
4. Kwanini mpaka sasa wahusika bado ni watu wasiojulikana
licha ya matukio kuendelea..?
5. Watoto saba waliokabidhiwa kwa jeshi la Polisi wako wapi
na taarifa yao kwanini haikutolewa..?
No comments:
Post a Comment