POLISI mkoani Arusha imewatia
mbaroni watu wawili wanaohusishwa na tukio la kuuawa kinyama kwa kuchinjwa
shingo kwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Ulinzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA), Stephen Kisamo.
Kifo
cha Kisamo kinahusishwa na mambo mengi yakiwemo vita ya kupambana na ujangili,
ikielezwa mkuu huyo alikuwa na siri nzito juu ya watu wanaojihusisha na
ujangili wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya Arusha, watumishi
wa serikali na wanasiasa.
Habari
kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Arusha zilieleza tayari imewatia ndani watu
wawili ambao ni marafiki wakubwa wa Kisamo na wanajua siri nzito kutokana na
kunaswa kwa mawasiliano ya simu ya kiganjani kati ya marehemu na watu fulani
muda mfupi kabla ya mauti kumfika ambao polisi inawachunguza kwa karibu.
“Wasiliana
na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas sisi tumeshakamata watu
wawili wa karibu na marehemu na sms na mawasiliano yanatia shaka, lakini ukweli
utajulikana muda si mrefu,” kilieleza chanzo chetu cha habari ndani ya Jeshi la
Polisi.
Kamanda
Sabas alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo Desemba 18, mwaka huu asubuhi
katika eneo la Kikwakwaru jijini Arusha muda mfupi baada ya Kisamo kutoka
nyumbani kwake akiwa na gari aina ya Mazda.
Sabas
alisema siku hiyo hiyo jioni alifika kituoni hapo mke wa marehemu na kueleza
juu ya kutoweka kwa mumewe ambapo mara moja polisi walianza kufuatilia jambo
hilo bila mafanikio.
Kamanda
Sabas alisema usiku, Polisi ilipokea taarifa kutoka kwa raia wema wa eneo hilo
la Kikwakwaru kuhusu kuonekana kwa gari hilo likiwa limeegeshwa maeneo hayo kwa
muda mrefu bila kuonekana mtu yeyote ambapo walifika na kulikuta gari hilo,
lililovutwa hadi katika Kituo Kikuu cha Polisi usiku huo na baadaye
lilitambuliwa na mke wa Kisamo.
Baadaye
walirejea eneo la tukio kwa lengo la kutafuta mwili wa marehemu huyo, lakini
hawakufanikiwa kuupata mwili wala kumuona kachero huyo ambapo walilazimika
kuomba ruhusa ya kupekua gari hilo.
Alisema
baada ya kuomba ruhusa hiyo, mke wa marehemu alipowasilisha ufunguo wa akiba wa
gari na Polisi walipofungua na kuanza upekuzi walikuta mwili wa marehemu ukiwa
umekunjwa kwenye buti, huku shingo yake ikiwa imechinjwa eneo la nyuma ya
shingo yake.
Aidha,
Kamanda Sabas alisema kwa mujibu wa maelezo ya mkewe, mumewe alikuwa mgonjwa na
alikuwa akijiandaa kwa safari ya India kwa matibabu, hivyo kabla ya tukio
walidhani alitekeleza gari baada ya kuzidiwa na ugonjwa.
Mwili
wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
No comments:
Post a Comment