WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
amefanya ziara nyingine ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na
kukagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa malipo baada ya kupewa
taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.
Waziri
Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi
Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu
nne (ICDs) ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo ni watumishi 10 tu ambao wamesimamishwa kazi kutokana na
makosa hayo. “Mmeamua kuwasimamisha kazi watu wadogo na kuwaacha wakubwa
wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha Serikali mapato namna hii,”
alisema Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu alimtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga amletee ofisini majina ya
watumishi wote, waliohusika na ukwepaji kodi huo ifikapo leo saa 11 jioni. Pia,
alimpa meneja huyo wiki moja, kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo
wa utozaji malipo kutoka kwenye billing system na badala yake kuweka mfumo wa
malipo wa kielektroniki (e-payment).
Alitoa
agizo hilo jana wakati akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari na kuona
ukaguzi wa mizigo, unavyofanyika kwa kutumia scanners. Akiwa kwenye chumba cha
scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja, ikisema kontena limejaa
diapers, lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner, ilionesha kuwa ndani ya
kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhdNYXcyZSnd661evR1qh1wfCC5uNEDgcd8pqeYh-SzdGY4yKWXgp3xCIpqh6GNSH-Ad2EdD_bvDqmzXgRRQ2GiCWWItj0LKK7ApSLQBNT6MsXL0TvpDLV_GZTYWtS5aClD47fSPkAi7hMp/s400/waziri.jpg)
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi
za Kampuni ya Reli (TRL) na kukagua mabehewa yaliyokuwepo, kisha akazungumza na
baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo, ambako alibaini madudu
kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.
Akizungumza
na Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Mhandisi Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika
kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji wao wa kazi, lakini anazo taarifa za
wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha Sh bilioni 13.5 ili waendeleze
miundombinu ya reli, lakini hawakufanya hivyo.
“Nia
ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha
kibiashara, lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema. “Ninazo taarifa
kuwa baada ya hapo, mlikopa shilingi bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili
kuendesha miradi ya shirika, lakini badala ya kufanya miradi, fedha hizo
mkaamua nazo kujilipa mishahara.
Sasa
sijui mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna mradi wowote uliofanyika,” alihoji
bila kupata majibu. Alipouliza wafanyakazi wana matatizo gani hapo TRL, Katibu
wa TRAWU, Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye mifuko
ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo ya kuanzia
Julai – Novemba 2014.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu alimtaka Mhandisi Mshana asimamie uboreshaji huduma za
usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam ili hata mabasi ya mwendo kasi
yatakapoanza, wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya usafiri
wautakao.
“Tunataka
kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu wenye magari, wawe wanayaacha huko na
kutumia usafiri wa treni au DART kuja mjini kama njia mojawapo ya kupunguza
msongamano wa magari jijini Dar es Salaam,” alisema.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment