Mkazi
wa Dar es Salaam, Dunia Salumu maarufu kwa jina la Dk. Manyaunyau, amehukumiwa
kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na kulipa fidia ya Sh milioni 10
baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha Sh milioni 29.6 kwa njia ya
udanganyifu.
Manyaunyau anadaiwa kujipatia kiasi
hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji, Tekra Modesta kama malipo ya kazi ya
kumfufua marehemu kaka yake aliyefahamika kwa jina moja la Modest ambaye
alifariki dunia miaka kadhaa iliyopita.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Flora Haule, alisema
mtuhumiwa huyo ametiwa hatiani baada ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa
mashtaka kujitosheleza.
“Mahakama inatoa hukumu kwa
mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa fidia ya Sh milioni
10 baada ya kumaliza kutumikia kifungo chake ili iwe fundisho kwa wengine wenye
tabia kama hizo,” alisema Hakimu Flora.
Upande wa mashtaka ulikuwa na
mashahidi wanne ambao wote waliithibitishia mahakama juu ya mtuhumiwa kujipatia
kiasi hicho cha fedha kwa njia za udanganyifu.
Awali Mwendesha Mashtaka wa
Serikali, Estar Kyala, aliiambia mahakama kuwa hakuna kumbukumbu za makosa ya
nyuma dhidi ya mshtakiwa na hivyo kuiomba kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho
kwa wote wenye tabia kama hizo.
Katika maelezo ya awali, ilidaiwa
kuwa mtuhumiwa alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji kama
malipo ya tukio la kutaka kumfufua kaka wa mlalamikaji.
Ilielezwa kuwa mtuhumiwa alipokea
fedha hizo kwa awamu mbili tofauti ambapo awali Mei 2007 jijini Dar es Salaam
alipewa kiasi cha fedha ambacho hakikufahamika.
Mei Mosi, mwaka 2008 mtuhumiwa
alipokea kiasi kingine cha fedha kama malipo kwa ajili ya kumalizia kazi yake
ya kumfufua marehemu ambaye ni ndugu wa mlalamikaji jambo ambalo alishindwa
kulitekeleza.
Manyaunyau amejizolea umaarufu mkubwa
katika maeneo mengi nchini kwa kile kinachodaiwa kuwa anao uwezo wa kutibu na
kuwafichua wachawi popote walipo sambamba na staili yake ya kunyonya damu ya
paka akiwa katika shughuli zake za uganga.
Katika tukio lililovuta wakazi wengi
wa Dar es Salaam, Manyaunyau anadaiwa kumwibua nyoka ambaye alikuwa tishio na
kuzusha hofu kubwa kwa wakazi wa maeneo ya Manzese Midizini ambapo ilidaiwa
kuwa alikuwa akiwagonga watu katika mazingira ya kutatanisha katika njia
inayopita kwenye makaburi.
Inaaminika kuwa baada ya kuitwa, Dk.
Manyaunyau aliweza kumuibua nyoka huyo na kuonekana hadharani tukio
lililohisiwa kuwa ni la kimazingara zaidi.
No comments:
Post a Comment