RAIS Jakaya Kikwete |
RAIS
Jakaya Kikwete amefanya uteuzi mbalimbali, ikiwemo wakuu wawili wapya wa mikoa.
Hatua hiyo inaziba nafasi zilizoachwa wazi na viongozi wa nafasi hizo,
wanaowania ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakuu wa mikoa wawili wapya
ni Amos Makalla, aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Jordan
Rugimbana, aliyepelekwa mkoani Lindi. Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ilieleza kuwa uteuzi huo wa Rais, umeanza Septemba
12 mwaka huu.
Wakuu wapya wa mikoa,
wataapishwa Septemba 16, Ikulu jijini Dar es Salaam. Taarifa hiyo iliyosambazwa
kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jana,
ilieleza kuwa katika uteuzi huo, Rais Kikwete pia amewahamisha wakuu wawili wa
mikoa, Mwantumu Mahiza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa
wa Tanga na Saidi Magalula amehamishiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akitokea
Mkoa wa Tanga.
Magalula anachukua nafasi
iliyoachwa wazi na Stella Manyanya, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, ambaye
sasa anawania ubunge jimbo la Nyassa mkoani Ruvuma kwa tiketi ya CCM.
Pia Manyanya alikuwa Mbunge
wa Viti Maalumu (CCM) akiwakilisha Mkoa wa Ruvuma. Makalla ni Naibu Waziri wa
Maji na alikuwa Mbunge wa Mvomero mkoa Morogoro, aliyemaliza muda wake.
Makalla anachukua nafasi
iliyoachwa wazi na Leonidas Gama, anayewania ubunge jimbo la Songea Mjini
mkoani Ruvuma kwa tiketi ya CCM. Rugimbana ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya
Morogoro anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na
Mahiza aliyehamia Tanga.
Kabla ya kuhamishiwa
Morogoro, Rugimbana aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es
Salaam. Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Profesa Muhammed Bakari Kambi
kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.
Kabla ya uteuzi Profesa Kambi
alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Shirikishi cha Muhimbili
(MUHAS), Dar es Salaam. Kikwete pia amemteua Dk Tulia Ackson kuwa Naibu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kabla ya uteuzi huo, Dk
Ackson alikuwa Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia,
Rais amemteua Victoria Mwakasege kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Kabla ya uteuzi wake,
Mwakasege alikuwa Naibu Balozi wa Tanzania nchini Burundi. Katika uteuzi wa
Rais, pia amewateua Makamishna wawili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Makamishna hao ni Mary
Longway na Asina Omari. Longway ni Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania na
Omari ni Wakili wa Kujitegemea. Makamishna hao wataapishwa Ikulu, Dar es Salaam
kesho. Rais pia amemteua Mlingi Mkucha kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la
Maendeleo ya Taifa (NDC).
Mkucha anachukua nafasi
iliyoachwa wazi na Gideon Nassari, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria. Aidha,
Rais amemteua Msaidizi wa Rais wa Diplomasia, Balozi Samwel Shelukindo kuwa
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa.
Katika uteuzi huo, pia
Kikwete amemteua Zuhura Bundala kuwa Balozi na Msaidizi wa Rais (Diplomasia)
kujaza nafasi iliyoachwa na Shelukindo. Kabla ya uteuzi wake, Bundala alikuwa
Mkurugenzi Msaidizi na Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Afrika.
Aidha, Rais amewateua
wakurugenzi wengine wanne wa wizara hiyo na kuwapandisha cheo kuwa mabalozi.
Walioteuliwa ni Abdallah Kilima ambaye anakuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya
Mashariki ya Kati.
Kabla ya uteuzi huo Kilima
alikuwa Ofisa Ubalozi Mkuu, Ubalozi wa Tanzania, Muscat, Oman. Wengine ni
Baraka Luvanda anayekuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Sheria. Kabla ya
uteuzi alikuwa Mratibu wa Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu.
Yumo pia Innocent Shiyo
anayekuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda. Kabla ya
uteuzi huo Shiyo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi katika Idara hiyo hiyo. Kikwete
amemteua Anisa Mbega kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora. Kabla ya
uteuzi wake alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Ubalozi wa Tanzania, Kampala, Uganda.
No comments:
Post a Comment