Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano
wa Jeshi la Polisi,
Advera Bulimba.
|
Jeshi la Polisi nchini linafanya uchunguzi kumbaini mmiliki
wa ukurasa wa twitter unaoendeshwa na anayejiita Daudi Balali, aliyewahi kuwa
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa
Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, aliyasema hayo wakati akizungumza na
Gazeti la Nipashe ofisini kwake jana.Bulimba alisema kuwa taarifa
za uwapo wa ukurasa huo wa twitter, wamekwishazipata na wanafanya uchunguzi wa
kina kumkamata mhusika kisha kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Tunazo taarifa juu ya ukurasa huo
wenye wafuasi wengi kwa sasa na unaotumika kuwashambulia viongozi wa serikali
na wa siasa hasa wale wanaogombea nafasi kubwa za utawala nchini, hivyo Jeshi
la Polisi lipo kwenye uchunguzi ili kumbaini mtu huyo haraka iwezekanavyo,” alisisitiza Senso.
Ukurasa huo ulioanza kutumika kabla
ya Sheria ya Uhalifu wa Mtandaoni kuanza kutumika, una wafuasi zaidi ya 6,000
kwa sasa na umekuwa ukitumika kuwachafua wagombea urais nchini hasa wa
upinzani.
Aidha, umekuwa ukitabiri matokeo ya
uchaguzi, kitendo ambacho kimekuwa kikiwachanganya wananchi.Bulimba alisisitiza
kuwa jeshi hilo liko makini na linafuatilia hivyo mtu huyo atasakwa na
kukamatwa akiwa mahali popote.
Aliwataka pia wananchi kuripoti
katika vituo vya polisi pindi wanapopata vitisho vya aina yoyote, kudhalilishwa
ama kufanyiwa kitu chochote kibaya kupitia mitandao ili wahusika wachukuliwe
hatua za kisheria.
“Jeshi la polisi linafanya kazi
usiku na mchana, hivyo mtu yeyote asijidanganye kwamba atavunja sheria na
asikamatwe, maana tuna njia nyingi za kuwabaini watu hao kwa kushirikiana vyema
na TCRA pamoja na wananchi, hivyo chanzo chochote kinachohusu uhalifu wa
mtandaoni, kitashughulikiwa,” aliongeza.
Aliwaonya pia watu waliokuwa
wakitumia kurasa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia majina ya
watu wengine ili kudhalilisha watu na kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo
juu ya masuala mbalimbali kuachana mara moja na tabia hiyo maana wakibainika
watachukuliwa hatua kali za kisheria na kuwa mfano kwa wengine wanaojihusisha
na vitendo hivyo.
Chanzo:Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment