KAMISHNA
WA OPERESHENI NA MAFUNZO YA JESHI LA POLISI AFANDE PAUL CHAGONJA
|
Ndugu zangu waandishi wa habari, nimewaiteni hapa kwa dharura, ili kuweza
kuwafahamisha hali halisi ya mauaji yaliyotokea katika siku za hivi karibuni
katika mkoa wa Kipolisi wa Tarime Rorya.
Mnamo tarehe 26 Januari, 2014 majira ya saa
12.00 asubuhi huko katika kijiji cha Mogabiri katika mkoa wa kipolisi Tarime
Rorya, jambazi asiyefahamika kwa jina aliwaua kwa risasi Zakaria Mwita Marwa
miaka 28 na Erick Lucas Maranya miaka 24 baada ya kukutana nao njiani.
Siku hiyohiyo, majiara ya saa 4:00 usiku, katika kijiji hichohicho cha
Mogabiri, jambazi huyo alimuua Robert Kisiri miaka 45 baada ya kuvamia Grocery
inayomilikiwa na Chacha Ryoba na kumjeruhi mtu mwingine mmoja.
Tarehe 27 januari, 2014 majira ya 11:30 alfajiri katika kijiji cha
Mugabiri, jambazi huyo alifanya mauaji tena kwa kumpiga risasi David Mwasi
Matiko miaka 39 na kumpora simu yake aina ya Nokia. Katika tukio hilo, pia,
alimjeruhi Machungu Nyamahemba miaka 19 ambaye bado amelazwa katika hospitali
ya Tarime kwa Matibabu.
Siku hiyohiyo ya tarehe 27 Januari, 2014 majira ya saa 2:00 usiku katika
kijiji cha Nkende, jambazi huyo alimuua kwa kumpiga risasi Juma Marwa Nyaitara
miaka 30. Baada ya kufanya mauaji hayo, jambazi huyo aliwapora simu zao za
mkononi Chacha Magige na Masero Marigiri wote wa kijiji cha Nkende.
Usiku wa kuamkia tarehe 28 Januari, 2014, jambazi huyo aliendelea kuua
watu wengine watatu ambao bado majina yao hayajafahamika. Mtu mmoja alipigwa
risasi wakati akiendesha pikipiki katika kijiji cha Nkende na wengine wawili
waliuawa baada ya kukutwa na jambazi huyo wakiwa wanatengeneza gari lililokuwa
limewaharibikia katika kijiji cha Mogabiri.
Hadi sasa juhudi kubwa za kumsaka jambazi huyo zinaendelea kufanyika na
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja
na wananchi. Aidha, mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernesti Mangu, ametuma
timu maalum kutoka makao makuu ya jeshi la Polisi inayohusisha kamisheni ya
Oparesheni, Upelelezi na Intelijensia kwenda kuongeza nguvu katika juhudi
zinazofanyika na ngazi ya mkoa kuhakikisha kwamba, jambazi huyo anakamatwa
upesi ili kuondoa hofu kwa wananchi.
Jeshi la Polisi nchini, linatoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano
ili jambazi huyo aweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria haraka.
Mwananchi mwenye taarifa za mhalifu huyo anaweza kutumia namba ya simu ifuatayo
0754 785557
No comments:
Post a Comment