MKUU WA WILAYA YA KOROGWE MRISHO GAMBO |
DIWANI wa Kata ya Mswaha-Darajani,
Tarafa ya Mombo, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga (CCM), Aweso Kipaku (34),
amejiuzulu nafasi hiyo akipinga hatua ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Mrisho Gambo,
kumuweka ndani.
Akizungumza na
mwandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Kipaku alisema Bw. Gambo aliagiza awekwe
ndani Januari 24 mwaka huu, saa 11 jioni na kupata dhamana saa nne usiku.
Alisema polisi walimkamata, kumpeleka Kituo cha Korogwe lakini Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani, alikwenda kumuwekea dhamana na kufanikiwa kutoka.
Mbali ya Kipaku, wengine waliokamatwa na kuwekwa ndani ni Ofisa Mtendaji Kijiji cha Mswaha-Darajani, Bw. Abbas Siafu na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mswaha-Darajani, Bw. Said Kijiwa.
Chanzo cha kukamatwa kwao ni tuhuma zilizotolewa dhidi yao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wakidaiwa kuchochea mgogoro wa wakulima na wafugaji kwenye Kijiji cha Mswaha-Darajani.
"Juzi tuliitwa kwa Mkuu wa Wilaya na viongozi wenzangu, baada ya kumalizika Kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Wilaya (Gambo) alimuamrisha OC-CID anichukue na kuniweka ndani hadi nilipopata dhamana usiku.
"Najiuliza mimi kiongozi wa wananchi nadhalilishwa kwa kufungwa pingu, kukaa chini tena nikisukumwa, je, wananchi wangu wapo salama kiasi gani... nimeamua kujiuzulu nafasi ya udiwani kwa vile nimedhalilishwa sana," alisema.
Kipaku
alisema tayari ametoa taarifa ya kujiuzulu kwake kwa Katibu wa CCM mkoani humo,
Gustav Muba jana ambapo zaidi ya wanachama 300 wa chama hicho wanaomuunga mkono
wamerudisha kadi.
Aliongeza
kuwa, sababu iliyomfanya awekwe ndani ni kitendo cha kuhudhuria Mkutano Mkuu wa
Kijiji uliofanyika Januari 21 mwaka huu na kudaiwa anachochea mgogoro wa
wakulima na wafugaji.
"Wakulima
wanataka wafugaji waondoke wakidai mifugo yao inakula mazao...Gambo aliahidi
angekwenda kusimamia kazi ya kuwaondoa wafugaji kwenye eneo husika lakini
hakufanya hivyo mara tatu, leo hii anasema sisi viongozi wa kata ndiyo tufanye
kazi hiyo kana kwamba tuna Jeshi la Polisi," alisisitiza.
Alisema
Januari 22 mwaka huu, watu wasiojulikana walikwenda kuchoma moto mazizi ya
wafugaji lakini chanzo si viongozi wa kata ni viongozi wa Wilaya na Mkoa ambao
wamechelewa kuchukua hatua za kumaliza mgogoro husika.
Juhudi za
Majira kumpata Bw. Gambo kuzungumzia sakata hilo zilishindikana ambapo juzi
alipigiwa simu lakini ilipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Alhajj Majid
Mwanga akidai wapo Tanga kwenye kikao na kuhoji mnataka kuzungumza na Mkuu wa
Wilaya kwa suala lipi.
Jana simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa ambapo Katibu wa CCM mkoani humo, Muba alikiri kupokea taarifa ya kujiuzulu diwani huyo lakini hakuwa tayari kuzungumza lolote akidai bado hawajajadili uamuzi wake kama wamkubalie au wamkatalie.
"Nimepewa
taarifa hiyo lakini tunasubiri barua rasmi, sisi kama chama lazima tumjadili na
turidhike na kile kilichofanya ajiuzulu, kama hakina mashiko tunajadiliana na
kumuomba aendelee kuwa diwani," alisema Muba
No comments:
Post a Comment