WAZIRI
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed
amemtaka Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (pichani)kutoa taarifa za kuwapo kwa
tishio la kundi la al Qaeda kuingia nchini kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili
vyombo hivyo, vishughulikie hatari hiyo.
Katika
mazungumzo yake na wanahabari hili, Aboud alisema kwa kuwa Lowassa anaelewa madhara
ya ugaidi na ana taarifa za kina kuhusu kundi hilo, ni vyema akazipeleka kwenye
vyombo vya usalama.
Mwishoni
mwa wiki, Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, alionya kuwa ipo hatari
Zanzibar ikatumiwa kuwa njia ya kuingia magaidi wa aina ya Al-Qaeda nchini.
Lowassa
alidai kuwa hilo linaweza kufanyika, endapo jitihada maalumu hazitafanyika sasa
katika kumaliza mkwamo wa kisiasa visiwani humo na kuzuia uwezekano wa
kuvunjika kwa hali ya amani.
Lakini,
Waziri Aboud aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika
Serikali ya Awamu ya Nne, alisisitiza kuwa Zanzibar ina amani na utulivu na
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imejipanga kuhakikisha hali ya
utulivu na amani inaendelea kudumu.
Alisema
SMZ itahakikisha inatekeleza agizo la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) la kufanyia
uchaguzi wa marudio na kuwapo kwa vitisho kutoka kwa baadhi ya vyama vya
upinzani.
Zanzibar
inatarajia kufanya uchaguzi wa marudio wa kuchagua Rais wa Zanzibar,
Wawakilishi na Madiwani Machi 20, mwaka huu, baada ya ule uliofanyika Oktoba
25, mwaka jana kufutwa siku tatu baadaye kwa tangazo la Mwenyekiti wa ZEC,
Jecha Salim Jecha kutokana na kuwapo kwa kasoro kadhaa.
ZEC
ipo katika maandalizi ya matayarisho ya uchaguzi huo huku ikitoa matangazo
kupitia vyombo vya habari kuwataka wananchi wenye sifa, kujitokeza kuomba
nafasi mbalimbali ikiwemo za uandishi katika vituo vya kupiga kura.
Katika
kilele cha maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM, yaliyofanyika Singida
mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Jakaya Kikwete
aliwataka wanachama na wafuasi wa CCM Zanzibar, kujiandaa na uchaguzi wa
marudio kwa ajili ya kukifanya chama hicho kuendelea na kushika dola.
No comments:
Post a Comment